Habari za Punde

KIPA WA KAGERA SUGAR DAVID BURHAN AFARIKI DUNIA, MECHI KAGERA V/S MTIBWA LEO KUAHIRISHWA?

KIPA aliyewahi kupata tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2013/2014, David Burhan amefariki dunia asubuhi ya leo katika hospitali ya Bugando, jijini Mwanza.

Kipa huyo aliyetokea Majimaji ya Songea alipotua akitokea Mbeya City na kujiunga na Wana Nkurukumbi Kagera Sugar ya Bukoba alifikishwa katika Hospitali ya Bugando baada ya kuugua ghafla jana akitokea Bukoba na kwa bahati mbaya asubuhi ya leo ameaga dunia.
Akithibitisha taarifa hizo kwa njia ya simu Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime, alisema kuwa Burhan, Burhan alikuwa anasumbuliwa na Malaria.
Aidha Mexime alisema matatizo hayo yalianza wakati wamekwenda Singida kucheza na wenyeji, Singida United mechi ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) katikati ya wiki.
Alisema alipanga kumuanzisha David Burhan katika mchezo huo, lakini hali yake ikabadilika ghafla hivyo akampanga kipa mwingine, Juma Kaseja badala yake.
“Tumecheza mechi, baada ya mechi wakati tunarudi, tunafika Biharamulo, macho yake yakaanza kubadilika yakawa ya njano, ikabidi alazwe pale, kesho yake akahamishiwa hospitali ya mkoa wa Kagera, ambako baada ya kupimwa wakasema apelekwe Bugando,”alisema Mexime.
Amesema uongozi wa Kagera Sugar ukafanya jitihada za haraka kumchukulia ndege kwenda Bugando Mwanza ambako alifika jana na kuanza matibabu kabla ya kufariki dunia leo asubuhi.
Mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kurejeshwa kwao Iringa na kuhusu mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Mexime amesema kwamba hawajajua kama utachezwa au la.
“Sasa hivi ndiyo tunakwenda kwenye kikao cha kabla ya mechi, Pree Match Meeting tukifika huko ndiyo tutajua, ila kwa kweli upande wetu wachezaji wote wameshitushwa mno na taarifa hizi na sidhani kama wapo tayari kwa mechi ya leo,”alisema.
Burham alijiunga na Kagera Sugar msimu huu akitokea Maji Maji ya Songea, ambayo nayo ilimtoa Mbeya City. Huyo ndiye aliyekuwa kipa wa kwanza Mbeya City wakati inapanda Ligi Kuu misimu mitatu iliyopita chini ya kocha Juma Mwambusi na akawa kipa bora wa msimu wa 2013/2014.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.