Habari za Punde

POLISI YANG’OA TAA KALI 665 ZA MAGARI ZISIZO SAHIHI

   Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Jeshi la Polisi Tanzania limeondoa taa za ziada (spot light) 665 zilizokuwa zimewekwa kwenye baadhi ya magari bila kupata kibali na utaratibu wa mtengenezaji wa chombo husika.
Hatua hiyo inalenga kupunguza ajali za barabarani zinazosababishwa na matumizi ya taa hizo zisizo sahihi.
Takwimu hizo zimetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, DCP Mohamed Mpinga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matumizi ya taa za gari.
DCP Mpinga alisema kuwa marekebisho yoyote katika gari yanahitaji kibali cha mtengenezaji , kinyume cha hapo ni uvunjaji wa sheria.
Aliongeza kuwa taa hizo hutumika vibaya hasa nyakati za usiku na kuwa chanzo cha ajali kwa sababu zinapotumika hupoteza uwezo wa mtumiaji  kuzitawala kwa maana ya kubadilisha uwakaji wake.

Kamanda Mpinga aliwashukuru baadhi ya watumiaji wa barabara kwa kuunga mkono usimamizi wa sheria kwa kuziondoa taa hizo kwa hiari na kuwasisitiza kuwa zoezi hilo ni endelevu hivyo waendelee kuzitoa taa hizo wenyewe.
Aidha, Kamanda huyo alitaja ajali za barabarani zilizotokana na matumizi mabaya ya taa kwa mwaka 2015 zilikuwa 104 na mwaka 2016 zilikuwa 123.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.