Habari za Punde

SERIKALI YATEKELEZA MKAKATI WA MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA

Na. JOVINA BUJULU – MAELEZO

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefanikiwa kukamilisha mkakati wa kitaifa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza wa mwaka 2013-2020.

Hayo yamesemwa jiji Dar es salaam na Mkurugenzi wa magonjwa yasiyoambukizwa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Profesa Ayoub Magimba.

Profesa Magimba amesema kuwa mkakati huo ni muendelezo wa utekelezaji wa maazimio ya vikao vya 66 na 68 vya Umoja wa Mataifa vilivyofanyika mwaka 2015 na 2016 ambapo Tanzania iliridhia kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

 “Katika kuimarisha huduma za kinga kwa magonjwa hayo, Serikali inatoa elimu kwa wananchi na kuwahimiza kufanya mazoezi, kupunguza matumizi mabaya ya pombe na sigara na kuhamasisha upimaji wa afya angalau mara mbili kwa mwaka,” alisema Profesa Magimba. 

Aliongeza kuwa mkakati huo  ambao umesambazwa nchi nzima kupitia kwa Waganga Wakuu wa Mikao yote unaainisha mikakati tofauti yenye malengo yanayoendana na malengo endelevu ya maendeleo ya melenia.

“Serikali imeimarisha tiba katika vituo vyote vya kutolea huduma kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na wataalamu, na kuimarisha huduma za Kibingwa za magonjwa ya moyo katika Taasisi za Bugando, KCMC, JKCI na ORCI,” Alisisitiza.

Profesa Magimba aliyataja magonjwa yasiyoambukiza kuwa ni pamoja na Saratani, magonjwa ya Moyo, magonjwa sugu ya njia ya hewa, Selimundu, magonjwa ya akili, Figo, Kisukari na baadhi ya magonjwa ya macho.

Akitolea mfano athari za magojnwa hayo, Profesa Magimba alisema kuwa utafiti uliofanywa katika ya mwaka 1994 – 2002 ulionyesha kuwa asilimia 18-24 ya vifo vilitokana na magonjwa yasiyoambukiza. 

Shirika la Afya Duniani lilikadiria kuwa asilimia 20 ya vifo vyote vilivyotokea hapa nchini mwaka 2005 vilitokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Takwimu zinaonyesha kuwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni tatizo la kimataifa ikijumuisha nchi za Afrika na nchi zinazoendelea.  Magonjwa hayo yamesababisha vifo million 36 duniani sawa na asiliamia 63 kwa kipindi cha mwaka 2008.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.