Habari za Punde

TTCL KUDHAMINI MASHINDANO YA SOKA LA UFUKWENI

Na. Lilian Lundo – MAELEZO
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) imedhamini mashindano ya Soka la ufukweni kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu vilivyopo Jijini Dar es Salaam yanayotarajiwa kufanyika katika fukwe za Coco Januari 07 mwaka huu.

Afisa Mkuu wa Mauzo kutoka Kampuni hiyo Peter Ngota ameyasema hayo leo, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya udhamini huo.

Aliendelea kwa kusema kuwa, mashindano hayo yanawalenga wanafunzi wa Vyuo Vikuu vilivyopo Jijini Dar es Salaam ambao ni wadau wakubwa wa Kampuni ya TTCL kupitia huduma ambazo wanazitoa kama vile vifurushi vya intanenti, dakika pamoja na ujumbe mfupi.

“Tumeamua kudhamini mashindano hayo kwa wanafunzi hao kutokana na umuhimu wa michezo kwao katika kuwajengea amani, furaha na afya njema ambavyo vitawawezesha kufanya vizuri katika masomo yao na hata kuwa wabunifu katika maeneo wanayosomea na kupelekea nchi kufikia uchumi wa kati,” alifafanua Ngota.

Kwa upande wake kocha Mkuu wa mashindano hayo John Mwansasu ameishukuru Kampuni ya TTCL kwa kudhamini mashindano hayo ambayo bado hayajapata umaarufu mkubwa hapa nchini.

Aidha amesema kuwa, ili kuwapa uzoefu washiriki wa mashindano hayo, kutakuwepo na wachezaji ambao walichezea timu za Simba na Yanga ambao pia watacheza kutokana na timu ambazo walikuwa wakichezea.

Vilevile Mwansasu amesema kuwa, wataendelea kushirikiana na Kampuni ya TTCL ili kusambaza mchezo huo katika mikoa yote ya Tanzania. 

Vyuo vilivyothibitisha ushiriki wa mashindano hayo mpaka sasa ni Chuo cha Biashara (CBE), Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu Huria (OUT), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT). Mashindano hayo hayatakuuwa na kiingilio na yataanza saa 3:00 asubuhi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.