Habari za Punde

VIJANA ASPIRE KWENDA SENEGAL, VIPAJI VINGINE VYATAFUTWA

Vijana watatu wa Tanzania ambao vipaji vyao vilitafutwa katika Mradi wa Aspire, wanatarajiwa kuondoka kesho Januari 5, 2017 kwenda Dakar, Senegal kwa ajili ya kujijunga na Akademi ya Aspire kuendelezwa kwa miaka mitano ijayo.
Vijana hao ni Ally Hamis wa Kituo cha Makongo, Dar es Salaam ambaye alizaliwa Septemba 16, 2003; Baraka Kadety wa Mzumbe, Morogoro aliyezaliwa Machi 11, 2003 na Martin Gabriel aliyezaliwa Julai 17, 2003 kutoka kituo cha Tabata, Dar es Salaam. 

Vijana hao walitafutwa mwaka jana katika vituo 14 za Aspire vilivyoko hapa nchini. Vituo hivyo viko mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Arusha na Kilimanjaro.
Mradi wa Aspire unaoendeshwa kwa ushirikiano wa Makao Makuu yalioko Qatar na Klabu ya Barcelona ya Hispania una lengo la kutafuta vipaji na kuvikuza katika vituo vyao. Kwa Bara la Afrika wana kituo Senegal (Dakar) wakati Makao Makuu yako Doha, Qatar.

Wakiwa Dakar, Senegal vijana hao wataendelezwa vipaji vyao pamoja na masomo na kwa kufanya kwao vema, watafanyiwa mipango ya kucheza soka la kulipwa katika nchi mbalimbali ambazo zimesonga mbele hususani Bara la Ulaya na Asia.
Wakati huo huo, Kocha Mmarekani George Kee anatarajiwa kuanza program yake ya kuanza kusaka vipaji Tanzania Januari 6, mwaka huu katika kituo cha Jakaya Kikwete kilichopo Kidongochekundu, Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
Kee ambaye ameshawishia kuja nchini na mmoja wa wachezaji wake chipukizi anayesoma Marekani, Mtanzania Masoud Abdul atakuwa katika kituo hicho kwa siku mbili mfululizo kwani siku nyingine ni Januari 7, mwaka huu.

Kwa kuanzia tu, program hiyo itaendelea Januari 8, mwaka huu huko Morogoro kabla ya kuamalizia programu hiyo Januari 9, mwaka huu huko Tanga. Vijana watakaopatikana, watafanyiwa mpango wa kwenda kusoma Marekani na kuendelezwa vipaji vyao katika akademi mbalimbali zinazosimamiwa na Kee.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.