Habari za Punde

ZAIDI YA WATU 90 WAPOTEZA MAISHA KWA MAFURIKO NCHINI THAILAND

Kituo cha kuzuia na kupunguza majanga ya kimaumbile nchini Thailand kimetangaza kuwa, watu 90 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kali zinazoendelea kunyesha katika mikoa 12 ya kusini mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na kituo hicho imeinukuu serikali ya Thailand ikisema kuwa, watu hao wamepoteza maisha kutokana na mvua hizo na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari kubwa kutokana na ongezeko la mafuriko, mawimbi makali ya bahari na kuendelea kunyesha mvua. Kituo hicho kimetangaza kuwa, hadi sasa mikoa saba ya kusini mwa nchi hiyo bado ina hali mbaya.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo jumla ya watu laki nane wameathiriwa na mvua hizo ambazo bado zinaendelea kunyesha. Hii ni katika hali ambayo kituo cha utabiri wa hali ya hewa kimetabiri kunyesha mvua kubwa ambazo zitakuwa kubwa zaidi katika maeneo ya kusini kuanzia leo Jumapili na kuendea kuyakumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. 
Utabiri huo pia umetahadharisha juu ya ongezeko la mawimbi makubwa yenye mwinuko wa zaidi ya mita mbili hadi tatu ambayo yatayakumba maeneo ya pwani ambayo hutembelewa sana na watalii.
Kufuatia hali hiyo, serikali imetuma maelfu ya askari kwa ajili ya kuwaokoa maelfu ya wakazi wa vijijini waliozingirwa na mafuriko sanjari na kukarabati barabara na madaraja katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.