Habari za Punde

BUNGE LAPITISHA MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALIMBALI

Na: Lilian Lundo – MAELEZO - Dodoma
Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania leo, Mjini Dodoma limepitisha muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali (Na. 4) wa mwaka 2016 [The written laws miscellaneous Amendments (No. 4) Bill, 2016].
Akiwasilishwa muswada huo Bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju amesema kuwa muswada huo unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria Sita ambapo lengo la marekebisho yanayopendekezwa ni kurahisisha utekelezaji wa Sheria hizo kwa kuondoa upungufu uliojitokeza wakati wa kutumia masharti ya sheria hizo.
Masaju alizitaja sheria zilizopendekezwa kufanyiwa marekebisho kupitia muswada huo kuwa ni Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana, Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Sheria ya Kodi ya Mapato, Sheria ya Ardhi,  Sheria ya Sukari na Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori.
“Ibara ya 21 ya muswada inapendekeza marekebisho katika kifungu cha 30 cha Sheria ambacho kinaweka masharti kuhusu Waziri mwenye dhamana ya fedha kukasimu madaraka yake chini ya Sheria hiyo. Sheria ilivyo sasa inaelekeza kuwa Waziri anaweza kukasimu mamlaka yake ya kujadili mkopo (negotiating loan), kuingia makubaliano ya kukopa mkopo na kutoa dhamana,” alifafanua Masaju.
Aliendelea kwa kusema kuwa muswada unapendekeza kuwa Waziri awe na uwezo wa kukasimu pia mamlaka ya kujadili au kuingia makubaliano ya misaada kwa mamlaka au mtu mwingine. Lengo la marekebisho hayo ni kurahisisha taratibu za upokeaji misaada kwa kuwa sheria hiyo ilikuwa kimya kuhusu suala hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa alipokuwa akitoa maoni na ushauri wa kamati hiyo alisema kuwa, kamati hiyo inaunga mkono marekebisho ya Sheria ya Mkopo wa Elimu ya Juu kwa sababu itatoa nafasi kwa Watanzania wengi wa kipato cha chini kupata nafasi ya kusoma katika Vyuo vya Elimu ya Juu.
Aidha ameeleza kuwa, kamati inakubaliana na mtazamo wa Serikali kwamba utoaji wa Mikopo ya Elimu ya Juu kwa ajili ya ngazi ya Diploma utazingatia vipaumbele vya Taifa kulingana na wakati husika.
Nae, Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa  amesema kuwa muswada huo umelenga kusaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata mikopo yenye riba nafuu.
Vile vile muswada huo unapendekeza marekebisho katika sheria ya Wanyamapori kuwa, katika hatua yoyote ya kesi ya Mahakama inaweza kwa kuamua yenyewe au kwa maombi  ya upande wa mashtaka kutoa amri kuwa mnyama, nyara ya Serikali, silaha, gari au kitu chochote kilichotolewa kama ushahidi ambacho kinaweza kuharibika au kupoteza thamani kiuzwe au kiharibiwe na Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Pia muswada huo unapendekeza kuongezwa kifungu kipya kitakachoweka masharti kuhusu bei elekezi ya miwa, sukari na bidhaa nyingine zitokanazo na miwa.
Mwenyekiti, Mhe. Najma Giga alitangaza rasmi kupitishwa kwa muswada huo na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupata kura nyingi za ndio. Aidha muswada huo unasubiri kibali cha Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili uanze kutumika kama sheria.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.