Habari za Punde

DKT. MGWATU AKAGUA UJENZI WA BOTI NNE ZA KISASA

Mtaalamu kutoka kampuni ya Songoro Marine Boatyard Ndugu Mohamed Salim (alie ndani ya boti) akimuelekeza jambo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu (wa kwanza kulia), pembeni yake ni Major Songoro pamoja na Meneja wa TEMESA mkoani Mwanza Mhandisi Ferdinand Mishamo. Boti hiyo ni moja kati ya mbili zinazotarajiwa kupelekwa maeneo ya Pangani mkoani Tanga pamoja na Msangamkuu mkoani Mtwara kwa ajili ya kutumika nyakati za dharura.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu (alieshika nguzo ya boti) akiangalia moja ya boti kati ya mbili yenye uwezo wa kubeba abiria nane zinazotarajiwa kupelekwa maeneo ya Pangani mkoani Tanga pamoja na Msangamkuu mkoani Mtwara kwa ajili ya kutumika nyakati za dharura.
Sehemu ya chini ya boti inayojengwa kwa ajili ya kutoa huduma mto rufiji katika eneo la Utete/Mkongo, boti hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 40. Ujenzi wa boti hiyo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu. Picha zote na Theresia Mwami TEMESA
***********************************************
Na Theresia Mwami TEMESA
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa boti nne za kisasa unaofanywa na kampuni ya Songoro Marine Boatyard jijini Mwanza. Akiwa katika karakana ya kampuni ya Songoro, Dkt. Mgwatu amesema kuwa Serikali imepanga kutekeleza mradi huo ili kutoa huduma za usafiri wa majini kwa wananchi katika maeneo manne tofauti.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni Pangani mkoani Tanga ambako wananchi walimuomba Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof. Makame Mbarawa alipokuwa akizindua Kivuko cha MV. Tanga kuwaletea boti ndogo itakayokuwa inatumika kuwasaidia wananchi wanapokuwa na dharura nyakati za usiku wakati ambapo kivuko cha MV. Tanga kinakuwa kimeegeshwa. Boti ya pili itapelekwa sehemu ya Msangamkuu mkoani Mtwara na vile vile itatumika kwa nyakati za dharura. Boti hizi mbili zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 8 kila moja.
Boti ya tatu itapelekwa eneo la Kilambo, Mtwara ambako kivuko cha MV. Kilambo kinatoa huduma ya kuvusha wananchi kati ya upande wa Tanzania na Msumbiji kupitia mto Ruvuma. Boti hii itatumika katika vipindi ambavyo maji ya mto ni machache kuweza kuendesha kivuko cha MV. Kilambo na itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 25.
Boti ya nne ambayo inajengwa kwa kutumia chuma itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 40 na itapelekwa kwenye eneo la Utete mkoani Pwani ili kiweze kutoa huduma wakati wote hata pale maji ya mto yanapokuwa machache. Nae Mkandarasi kutoka kampuni ya Songoro Marine Boatyard, Bw. Major Songoro amesema kuwa kazi ya kujenga boti zote nne inatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Dkt. Mgwatu alikuwa katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza kukagua na kujionea maendeleo ya ujenzi wa boti hizo nne.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.