Habari za Punde

LIGI KUU TANZANIA BARA KUENDELEA TENA WIKI HII, YANGA KUJIULIZA KWA RUVU SHOOTING

 Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), inatarajiwa kuendelea keshokutwa Jumatano huku mabingwa watetezi wa taji hilo, Young Africans itaalikwa na Ruvu Shooting kwenye mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mbali ya mchezo huo mmoja kwa siku ya Jumatano, ligi hiyo ambayo ni michuano mikubwa nchini, pia itaendelea mwishoni mwa wiki hii kwa siku ya Jumamosi Machi 4, mwaka huu kwa kuwakutanisha Simba na Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Michezo mingine ya Jumamosi Machi 4, mwaka huu itakuwa ni kati ya Toto Africans na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza huku Kagera Sugar wakiikaribisha Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Azam FC pia itakipiga na Stand United ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Chamazi siku hiyo ya Jumamosi Machi 4, mwaka huu, ambapo  Mchezo huo utaanza saa 1.00 jioni wakati mechi nyingine zitaanza saa 10.00 jioni.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limerejesha tena mechi za Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Jumapili Machi 5, mwaka huu Mtibwa Sugar itaialika Young Africans kwenye uwanja huo katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
 Mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya Vodacom utachezwa Uwanja wa Uhuru ambako African Lyon itaialika Mwadui ya Shinyanga wakati Ndanda FC itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.