Habari za Punde

MAHAKAMA KUU YATOA ZUIO LA KUTOMKAMATA WALA KUMTIA KIZUIZINI FREEMAN MBOWE


MAHAKAMA kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa zuio la muda kwa polisi kutomkamata Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, hadi hapo maombi yake ya kutaka kutokamatwa na kuwekwa kizuizini yatakaposikilizwa  na kutolewa uamuzi na Mahakama.
Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Sekieti Kihiyo, Lugano Mwandambo na Pellagia Kaday.
Hata hivyo Mahakama imewaambia Polisi waendelee na uchunguzi wao wakati wowote na kama kawaida pindi watakapokuwa wanahitaji kufanya hivyo.
Aidha mahakama kuu pia imewaruhusu upande wa mlalamikaji, (Mbowe)  kufanyia marekebisho hati yao ya wito na kumuongeza Mwanasheria mkuu wa Serikali katika kesi hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali Mkuu Gabriel Malata kusimama na kuwawakilisha wajibu maombi ambao ni mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Dar es Salaam, Simon Sirro na Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Camilius Wambura.
Kabla ya kukubaliwa kuwawakilisha wadaiwa, jopo la mawakili wa mlalamikaji, wakiongozwa na Tundu Lissu, walitaka kupinga Malata kuwawakilisha wadaiwa akidai kuwa walitakiwa kusimama mwenyewe mahakamani kwa kuwa hawakuwa wamemuhusisha Mwanasheria mkuu.
Malata alipinga hoja hiyo na kusema yeye yupo kwa ajali ya serikali, hata kama AG hayumo.
" Kwa sababu hajashtakiwa Makonda yeye Binafsi wala Sirro Bali ni mkuu wa Mkoa na Kamanda wa Polisi, basi ninayo mamlaka ya kuwawakilisha". Amesema Malata.
Kufuatia hali hiyo Lissu aliiomba mahakama kufanyia marekebisho ya hati yao ya wito na kumuongeza AG ombi ambalo court ilikubaliana nalo na kuwaamuru wafaili hayo marekebesho jumatatu (Feb.27).
Kesi hiyo itatajwa March 8, mwaka huu.
Mbowe alitakiwa kuripoti Kituo cha Polisi Kati baada ya jina lake kutajwa miongoni mwa majina yaliyotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda katika awamu ya pili ya watu wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.