Habari za Punde

NAPE AIPONGEZA SERENGETI BOYS KWA KUFUZU FAINALI ZA AFCON GABON 2017

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye ametuma salamu za pongezi kwa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa vijana wenye chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) kwa kufuzu Fainali za Mashindano ya Africa kwa vijana chini ya umri wa miaka 17.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa miguu barani Afrika (CAF) imeeleza kuwa Serengeti Boys inafuzu fainali hizo mara baada ya kushinda kwa rufaa yao dhidi ya Timu ya Congo Brazaville ambapo timu hiyo ilimchezesha mchezaji Langa Lese aliyezidi umri wa miaka 17.
Mhe. Nape amesema kuwa, hiyo ni fursa kubwa ambayo Tanzania imeipata katika mashindano ya kimataifa na kuna kila uwezo na sababu ya kushinda na kuchukua kombe hilo.
Waziri Nape ametoa shukrani zake za dhati kwa watanzania na wadau wa michezo kwa michango yao ya hali na mali iliyoifanya Serengeti Boys kufikia hapa ilipofika na kuzidi kuendelea kuiunga mkono kwa hali na mali timu hiyo katika kuelekea fainali hizo.
Mhe. Nape Moses Nnauye amewatakia mafanikio Serengeti Boys kuelekea katika Fainali za michuano ya AFCON zitakazofanyika nchini Gabon Aprili, 2017.
Imetolewa na:
Zawadi Msalla 
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo.
03/02/2017

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.