Habari za Punde

SAKATA LA MANJI YAIBUKA MAPYA, SASA NI LA KUMILIKI PASIPOTI MBILI

Na Mwandishi Wetu, Dar
ASKARI wa Idara ya Uhamiaji Tanzania wapo nje ya wadi ya wagonjwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wakimsubiri Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji aruhusiwe wamtie nguvuni.
Inadaiwa Uhamiaji wanataka kumtia mbaroni Manji kwa kosa la kumiliki pasipoti mbili, jambo ambao ni kinyume cha Sheria.
Manji amelazwa JKCI tangu Alhamisi jioni alipoachiwa kwa dhamana baada ya kusomewa shitaka la tuhuma za kutumia dawa za kulevya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Kesi hiyo iliyoanzia kwa Hakimu Cyprian Mseha, imeahirishwa hadi Machi 16 kwa mwendelezo wa kesi hiyo.
Ikumbukwe Manji aliwasili mahakamani chini ya ulinzi wa Polisi, akitokea kituo kikuu cha Polisi, Dar es Salaam alikuwa amewekwa rumande tangu Februari 9, mwaka huu.
Mwenyekitiwa Yanga, Yussuf Manji yupo katika wakati mgumu kwa sasa.

Hata hivyo, Februari 11 mchana Manji alipelekwa JKCI baada ya hali yake kubadilika na kuwa mbaya ikiwelezwa anasumbuliwa na matatizo ya moyo.
Taarifa zilisema Manji alifanyiwa upasuaji mdogo na kurejeshwa Polisi Februari 15, kabla ya siku iliyofuata kupandishwa kizimbani. 
Manji aliwekwa rumande baada ya kujisalimisha mwenyewe kituo kikuu cha Polisi Februari 9, baada ya kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika orodha ya watu 65 wanaoshukiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Japokuwa Manji na wengine wote 64 waliotajwa walitakiwa kuripoti Polisi Februari 10, lakini yeye alijipeleka mwenyewe siku moja kabla pamoja na Askofu Gwajima, ambaye aliachiwa baada ya siku mbili.
Na wakati tuhuma zake zikibadilika kutoka kwenye kushukiwa kuuza hadi kudaiwa anatumia dawa za kulevya, Manji pia anakabiliwa na shitaka lingine kupitia kampuni yake ya Quality Group Limited, kuajiri wageni bila vibali vya kufanya kazi nchini.
Ofisa wa Idara ya Uhamiaji Dar es Salaam, John Msumule, alisema Februari 14 kwamba Manji anatakiwa kufika ofisini hapo kujibu mashitaka ya kuajiri watu 25, ambao hawana vibali vya kufanya kazi nchini. 
Msumule alisema ilikuwa wamkamate Manji Februari 13, lakini wakaambiwa amelazwa hospitali, hivyo wameacha maagizo akitoka hospitalini aripoti mwenyewe Ofisi ya Uhamiaji makao makuu Dar es Salaam.
Msumule alisema kwamba walifanikiwa kukamata pasipoti 126 zenye makosa Jumamosi na kati ya hizo, 25 zilikuwa za waajiriwa ambao hawana vibali.
Na sasa askari wa Uhamiaji wapo nje ya wadi ya JKCI wakimsubiri Manji aruhusiwe ili wamtie nguvuni na kurudishwa Rumande kwa mashitaka mengine. Source Bin Zubeiry

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.