Habari za Punde

SERIKALI YAIPONGEZA AZAM MARINE KWA KUTOA HUDUMA YA USAFIRI KATI YA PEMBA NA TANGA

Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.
Serikali kupiti Bunge lake Tukufu limetoa pongezi kwa kampuni ya Azam Marine kwa kuanza kutoa huduma za usafiri kati ya Mkoa wa Tanga na Pemba.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani alizitoa pongezi hizo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tanga Mjini juu ya mpango wa Serikali wa kununua meli ya kisasa na ya uhakika ili kuokoa wasafiri wa Tanga na Pemba.
“Tarehe 29 Januari, 2017 kampuni ya Azam Marine imeanza kutoa huduma ya usafiri wa abiria na mizigo kati ya Pemba na Tanga kwa kutumia Meli ya Sealink 2 yenye uwezo wa kubeba abiria 1,650 na mizigo tani 717,” alifafanua Mhandisi Ngonyani.
Aliendelea kwa kusema kuwa Januari 31, 2017 Meli ya Sealink 2 iliondoka Tanga saa 3:00 asubuhi kwenda Pemba hadi Unguja. Aidha Meli hiyo itafanya safari zake mara moja kwa wiki baina ya Pemba na Tanga hadi pale ambapo idadi ya mizigo itakapolazimu kuongeza safari nyingine.
Mhandisi Ngonyani amesema kuwa Serikali inaipongeza kampuni hiyo kwa kuitikia wito wa kuanzisha huduma ya usafiri majini baina ya Tanga, Unguja na Pemba hivyo kuondokana na changamoto za usafiri zilizokuwa zikiikabiri mikoa hiyo.
Aidha ametoa wito kwa wawekezaji wengine kupeleka vyombo vya usafiri vya kisasa majini ili kuongeza huduma ya usafiri katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya usafiri kupitia njia ya majini.
Vile vile amewataka wananchi wanaosafiri kati ya Pemba na Tanga kutumia huduma za meli salama na kuachana na vyombo visivyo salama vinavyo hatarisha maisha na mali zao.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.