Habari za Punde

SIMBA YASHINDA 'VITA YA MAJIMAJI' UGENINI YAIBANJUA 3 - 0Na Mwandishi Wetu, Songea
TIMU ya Simba leo imeibuka na ushindi wa mabao 3- 0 dhidi ya Majimaji ya Songea katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa jioni hii kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Kwa ushindi huo wa leo Simba sasa wamepunguza gepu la wapinzani wao Yanga walioshinda jana na kuongoza kwa tofauti ya pointi 4, na leo kubakisha tofauti ya Pointi 1.
Simba ilianza mbio za ushindi katika dakika ya 20 kwa bao lililofungwa na IbrahimAjibu.
Bao la pili lilifungwa na Said Ndemla na la tatu kupitia kwa Mrundi Laudit Mavugo.
Kocha wa Simba Joseph Omog alifanya mabadiliko katika mchezo huo, ambao mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa ruvu, Dk Binilith Mahenge baada ya kuwatoa Jamal Mnyate na kumuingiza Pastory Athanas.
Kocha wa Majimaji, Kally Ongala baada ya mchezo huo aliwalaumu wachezaji wake kwa kucheza chini ya kiwango, ambapo alisema kipigo hicho ni cha kujitakia.
Alisema wachezaji wake walishindwa kufuata maelekezo tofauti na walivyocheza dhidi ya Ndanda ya Mtwara na kusababisha kupoteza mchezo huo.

Naye Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo, ambapo alisema wamecheza vizuri kwa kufuata maelekezo.
Mayanja aliwaahidi wapenzi wa Simba kuwa makosa ya nyuma hayatajirudia katika mechi zijazo, ambapo sasa ni mwendo mdundo na wataendelea kushinda kila mechi iliyo mbele yao.

Wakati huohuo, Azam FC usiku wa leo inawakaribisha Ndanda FC katika mchezo mwingine utakaopigwa kwenye Uwanja wa Chamazi Mbagala jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.