Habari za Punde

TANZIA: KIUNGO WA ZAMANI WA YANGA NA TAIFA STARS GODFREY BONNY AFARIKI DUNIA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya kutokana na kifo cha mchezaji wa zamani Tanzania Prisons, Young Africans na timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Godfrey Bonny.

Taarifa zilizothibitishwa na uongozi wa Mkoa kutoka Mbeya, zinasema kwamba mchezaji huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia leo Ijumaa Februari 17, 2017 kwenye Hospitali ya Wilaya ya Rungwe, ambako alikuwa amelazwa tangu Feb 7 mwaka huu, akisumbuliwa na kifua.

TFF itawakilishwa na Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya, Seleman Haroub ambaye kwa sasa atashirikiana na familia kufanya taratibu za mazishi ambayo taarifa zaidi zitatangazwa baadaye mara baada ya vikao vya familia.

Katika salamu zake za rambirambi, TFF imewataka ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu kuwa na uvumilivu kwa kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito kwa Bonny ambaye nyota yake iling’ara zaidi wakati Taifa Stars inafundishwa na Mbrazil Marcio Maximo. 
Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.