Habari za Punde

TEA YASAINI MAKUBALIANO YA KUHIFADHI MIRADI YA ELIMU NA KAMPUNI YA SUNSHINE GROUP LTD

 Kaimu Mkurugenz Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Graceana Shirima na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sunshine Group Ltd  Sun Tao wakisaini mkataba wa makubaliano wa kufadhili miradi mbalimbali ya elimu kwa shule za Msingi na Sekondari leo Jijini Dar es Salaam.   Miradi hiyo ni ujenzi wa madarasa, mabweni, viwanja vya michezo, vifaa vya kujifunzia na vifaa vya maabara itakayotekelezwa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Mara na Mtwara   
Kaimu Mkurugenz Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Graceana Shirima na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sunshine Group Ltd  Sun Tao wakibasilishana mikataba ya makubaliano wa kufadhili miradi mbalimbali ya elimu nchini mara baada ya kumaliza kuisaini leo jijini Dar es Salaam.
Watumishi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Kampuni ya Sunshine Group Ltd wakiwa katika picha ya pamoja.
*************************************************************
Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imesaini makubaliano ya kufadhili miradi mbalimbali ya elimu nchini na Kampuni ya Kichina ya Sunshine Group Limited.
Miradi itakayotekelezwa katika makubaliano hayo ni miundombinu na vifaa vya kujifunzia pamoja na vifaa vya maabara kwa shule za Msingi na Sekondari hapa nchini.
Makubalino hayo yamesainiwa leo, Mjini Dar es Salaam kati ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TEA Graceana Shirima na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sunshine Group Ltd Sun Tao, ambao utahusisha  shule zilizopo mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Mara na Mtwara.
“Miradi ya kwanza kutekelezwa kupitia makubaliano haya ni ujenzi  wa maabara mbili za Sayansi katika Shule ya Sekondari Matundasi iliyopo katika Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya na kujenga madarasa na miundo mbinu ya maji katika shule ya Sekondari Bunda, iliyoko mkoani Mara ambayo itagharimu zaidi ya Shilingi Milioni 220,” alisema Graceana Shirima.
Aliendelea kwa kusema  kuwa miradi itakayotekelezwa na Kampuni hiyo ni ujenzi wa madarasa, mabweni, viwanja vya michezo, kutoa vifaa vya michezo, kutoa vifaa vya kujifunzia pamoja na vifaa vya maabara ambayo itatekelezwa kupitia Mfuko wa Elimu unaosimamiwa na Mamlaka hiyo.
Vile vile amesema kwamba, makubaliano hayo ni ya miaka mitano na baada ya miaka hiyo mitano watapitia tena makubaliano hayo ili kujiridhisha ikiwa yatafaa kuendelea.
Kwa upande wake Sun Tao amesema kuwa Kampuni  yao inajihusisha  na miradi mbalimbali hapa nchini ikiwemo viwanda vya kuchakata korosho vilivyoko Lindi na Mtwara, Kiwanda cha Mafuta ya Alizeti kilichopo Dodoma, uchimbaji wa Madini Mkoani Chunya  na masuala ya miundo mbinu.
Aidha amesema kuwa wameanza kwa kutoa ufadhili kwa mikoa ambayo Kampuni yao ina miradi ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Mara na Mtwara na baadae wataendelea kutoa ufadhili kwa mikoa mingine iliyobakia  ili kuboresha mfumo wa elimu nchini.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.