Habari za Punde

VIJANA CHANGAMKIENI PROGRAMU YA KUKUZA UJUZI

 Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Robert Masingiri akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini inayoratibiwa na Ofisi hiyo. Kushoto ni Afisa Habari wa Ofisi hiyo Bw. Ridhiwani Wema.
 Afisa Habari Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Ridhiwani Wema akiongea na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ajira kutoka Ofisi hiyo Bw. Robert Masingiri Picha na Fatma Salum-MAELEZO
**********************************************************
Na Fatma Salum – MAELEZO
Serikali imetoa wito kwa vijana kote nchini kuchangamkia fursa ya kupata ujuzi wa fani mbalimbali kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Robert Masingiri wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu programu hiyo.
Masingiri alibainisha kuwa programu hiyo ni muhimu kwa vijana kwani itawawezesha kupata ujuzi na stadi stahiki ili kumudu ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
“Utekelezaji wa programu hii ni hatua za makusudi za Serikali za kukabiliana na kiwango kidogo cha ujuzi miongoni mwa nguvu kazi ya Taifa.” Alisema Masingiri.
Aliongeza kuwa kiwango cha ujuzi hakijafikia hatua nzuri ya kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati hivyo Serikali imetenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya programu hiyo na utekelezaji wake umeanza mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2020/2021
“Programu hii inalenga kuziba pengo kubwa lililopo la ukosefu wa ujuzi katika sekta za utalii, ujenzi, viwanda, nishati na madini ambapo utawawezesha vijana wengi kuajirika na kujiajiri.” Alisema Masingiri.
Akifafanua kuhusu mfumo wa utekelezaji wa programu hiyo, Afisa Habari kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Ridhiwani Wema alisema kuwa programu hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali kwa njia ya uanagenzi (apprenticeship) ambapo lengo ni kuwafunza vijana 3000 katika viwanda vya nguo na vijana 1000 katika sekta ya ngozi.
Wema aliongeza kuwa program hiyo pia inatekelezwa kupitia urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi (Recognition of Prior Learning) na vijana 3900 watarasimishwa kupitia sekta ya ujenzi, utalii na ukarimu.
Aidha kupitia program hiyo wahitimu 4000 watapata mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi na wafanyakazi 13400 watapatiwa mafunzo ya kuongeza ujuzi.
“Ofisi ya Waziri Mkuu imesaini mikataba na VETA na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) ili watoe ujuzi kwa vijana kote nchini na kupitia programu hiyo mafunzo hayo yanagharamiwa na Serikali , hakuna malipo.” Alieleza Wema.

Serikali imejipanga kuendelea kukamilisha miongozo ya ukuzaji ujuzi kwa njia mbalimbali itakayowezesha wadau kushiriki katika utekelezaji wa Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini ili kufikia sera ya kukuza viwanda na kujenga uchumi wa kati.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.