Habari za Punde

VIPINDI MAALUM VYA RADIO KUPINGA UKATILI VYAZINDULIWA

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bi. Sihaba Nkinga akikata utepe kuashiria mwanzo wa urushaji vipindi maalumu vya kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
*******************************************
Wizara ya Afya, Idara kuu Maendeleo ya Jamii leo imezindua wa vipindi maalumu vya Radio ambavyo vinalenga kuelimisha jamii kuacha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto hapa nchini. 

Vipindi hivi vitakuwa vikirushwa na Radio maalufu nchini ‘RADIO TIMES 100.5 FM ambayo itashirikiana na wataalamu wa Wizara kusimamia na kuratibu maandalizi ya uendeshaji wa vipindi vya elimu na stadi za kuzuia ukatili wa kijinsia katika jamii. 
Akaiongea katika sherehe fupi ya uzinduzi wa vipindi hivyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Idara kuu Maendeleo ya Jamii Bi. Sihaba Nkinga amesema ubunifu wa vipindi hivi na Radio Times 100.5 ni sehemu ya mwitikio wa tasnia ya habari katika kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto ambao ulizinduliwa Desemba, 2016. 

Ameongeza kuwa uzinduzi wa vipindi maalum vya elimu kwa umma ni kielelezo thabiti kwamba RADIO TIMES FM inadhamira ya dhati ya kusaidia juhudi za Serikali kuimarisha ulinzi na usalama wa mama na mtoto. 
Bi Sihaba aliendelea kusema kuwa anatambua kuwa REDIO TIMES FM ni chombo binafsi ambacho kimetambua kuwa kinaowajibu wa kuhakikisha kuwa wanawake na watoto katika nchi yetu wanafurahia upatikanaji wa haki zao na wanaishi katika mazingira salama. 
Pia amewapongeza wanahabari wa vyombo vyote vinavyoelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu athari za ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kujadili afua zinazotakiwa kuchukuliwa katika kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto na madhara ya ukatili huo. 
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bi. Sihaba Nkinga akijiweka tayari kurusha kipindi maalumu cha kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
****************************************************
Aidha ametoa rai kwa vyombo vingine vya habari kufuata nyayo za Radio Times FM katika kukuza uelewa wa jamii kuhusu athari za ukatili dhidi ya wanawake na watoto. 
Katibu Mkuu huyo ametaja ukatili kuwa na athari ambazo huwapunguzia uwezo wanawake na watoto katika kupata haki ya kushiriki shughuli za uzalishaji kwa uhuru na amani huku akaizitaja takwimu za Jeshi la Polisi kuwa zinaonesha vitendo vya ubakaji kwa mwaka 2015 vilifikia 3,444 na matukio ya shambulio, kujeruhi na matusi vilikuwa14,561. 

Aidha utafiti wa Idadi ya Watu na Afya ya mwaka 2010 inaonesha kuwa asilimia 39 ya wanawake wa umri wa miaka 15 – 49 walifanyiwa ukatili wa shambulio na vilevile Taarifa ya Utafiti wa Ukatili dhidi ya Watoto ya mwaka 2011 ilibainisha kuwa asilimia 72 ya wasichana na asilimia 71 ya wavulana nchini walifanyiwa ukatili wa vipigo. 

Taarifa hiyo pia imebainisha kuwa mtoto 1 kati ya watoto 3 wa kike na mtoto 1 kati ya watoto 7 wa kiume walifanyiwa ukatili wa kingono. Aidha, takwimu zinaonesha kuwa watoto 15 kati ya watoto 100 wa kike hapa nchini wamefanyiwa ukeketaji.
Kwa ujumla takwimu hizi zinaonesha jinsi gani tatizo hili lilivyokubwa katika jamii zetu, hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuchukua hatua thabiti kuzuia ukatili huo aliendelea kusema.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.