Habari za Punde

WANAFUNZI WALIOSOMA SHULE YA SEKONDARI ILULA WILAYA YA KILOLO WACHANGIA UKARABATI WA SHULE

Wawakilishi wa wanafunzi waliosoma shule ya sekondari Ilula katika wilaya ya Kilolo mkoani Iringa Mwalimu Nguvu Chengula kushoto na mchungaji Yekonia Koko wakimkabidhi fedha kiasi cha Tsh milioni 1.3 mkuu wa shule ya sekondari Ilula mwalimu Vincent Shauri (katikati) kulia ni makamu mkuu wa shule hiyo Joachim Mlay
Mkuu wa shule ya Sekondari Ilula katikati akiwaonyesha choo cha kisasa kinachojengwa shuleni hapo kwa ajili ya matumizi ya walimu . KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Mkuu wa shule ya Sekondari Ilula Vicent Shauri kulia akionyesha choo hicho. 
***********************************************
Na Mwandishi Wetu, Iringa
WANAFUNZI waliosoma shule ya sekondari Ilula wilayani Kilolo mkoa wa Iringa wametoa msaada wa fedha kiasi cha Tsh milioni 1.3 kwa ajili ya kuchangia ukarabati wa shule hiyo baada ya kukumbwa na maafa ya kuezuliwa na kimbuka vyumba vya madarasa na bweni la wanafunzi.
Wakikabidhi maasada huo mchungaji Yekonia Koko na Mwalimu Nguvu Chengula jana kwa niaba ya umoja wa wanafunzi waliosoma katika shule hiyo walisema kuwa wameguswa na changamoto mbali mbali zilizopo katika shule hiyo hasa baada ya kupatwa na maafa ya vyumba vya madarasa na bweni kuezuliwa na kimbunga na kupelekea wanafunzi kuendelea kulala darasani kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.
Hivyo walisema kupitia umoja wao wanafunzi waliosoma katika shule hiyo wamelazimika kuchangishana fedha ili kusaidia uboreshaji wa shule hiyo kama sehemu ya mchango wao kwa shule hiyo pia njia moja wapo ya uhamasishaji wa wananchi kuendelea kuchangia maendeleo ya elimu badala ya kuiachia serikali .
Alisema Chengula kuwa baada ya serikali kufuta ada katika shule ya msingi na sekondari wananchi wanao wajibu wa kushiriki kuchangia maendeleo ya shule hiyo kama ujenzi na ukarabati wa shule kwani pasipo kufanya hivyo shule nyingi zitabaki magofu kutokana na baadhi ya wananchi kuwa na dhana potofu kuwa hawapaswi kuchangia maendeleo ya elimu .
Chengula ambae ni mkurugenzi wa shule ya Sun Academy mjini Iringa alisema kuwa ili jamii iweze kunufaika na ubora wa elimu inayotolewa nchini ni lazima mazingira ya ufundishaji na mashule kuboreshwa na njia pekee ya kuboresha ni pamoja na wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi wa shule ikiwa ni pamoja na kuwa na harambee za mara kwa mara kwa ajili ya kuboresha majengo ya shule .
" Shule hii hii imetoa wanafunzi wengi sana ambao baadhi yao kwa sana wanafanya kazi katika maeneo mbali mbali na baadhi yao wameanzisha shule zao binafsi kama ilivyo kwangu mimi, ila shule hizi ambazo zimetuwezesha hadi kufika hapa zina changamoto nyingi zikiwemo za uchakavu wa majengo jukumu letu ni kurudisha shukrani kwa shule tulizosoma kwa kuchangia maendeleo ya shule hizi ili wanafunzi wasome katika mazingira mazuri zaidi"
Hata hivyo alisema inasikitisha kuona wanafunzi wanaendelea kulala darasani kutokana na bweni lao kuezuliwa na kimbunga na kuwa kuna haja ya serikali ya wilaya ya Kilolo na wadau kufanya jitihada za kuboresha miundo mbinu ya bweni hilo ili kuwawezesha wanafunzi kurejea katika bweni badala ya kuendelea kulala darasani.
Kuhusu wanafunzi waliosoma katika shule hiyo na sasa wanafanya kazi katika taasisi na wengine kuwa na taasisi zao aliwataka kukutana na kuangalia uwezekano wa kupeana majukumu ya kuchangia uboreshaji wa shule hiyo kama ambavyo wachache wao walivyoanza kuchangia kwa ajili ya uboreshaji wa shule hiyo.
Wakati mchungaji Koko alieleza kusikitishwa kwake na miundo mbinu mibovu ya umeme iliyopo katika shule hiyo na kuwa pasipo shirika la umeme nchini (Tanesco) wilaya ya Kilolo na mkoa wa Iringa kuchukua jitihada za haraka upo uwezekano wa shule hiyo kukumbwa na maafa siku za mbeleni .
Kwani alisema inasikitisha kuona nguzo ambazo zimepeleka umeme katika mabweni ya wanafunzi kuwa za kienyeji ambazo zimewekwa na uongozi wa shule hiyo na umeme unaotumika shuleni hapo kuwa umeme wa kiwango cha chini zaidi baada ya kuwekewa umeme wa njia mbili badala ya njia tatu ambao umewezesha shule hiyo kuwa na uhakika wa umeme.
Mkuu wa shule hiyo Vecent Shauri mbali ya kuwashukuru wanafunzi hao waliopata kusoma katika shule hiyo kwa kusaidia kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo bado alisema tayari uongozi wa shule hiyo ulijaza fomu TANESCO kuomba kufikishiwa umeme wa uhakika na kuwa ni nguzo tatu pekee zinahitajika ila hadi sasa zaidi ya miaka mwaka mmoja hawajafika kusogeza umeme katika shule hiyo.
Akitoa taarifa ya uchakavu wa majengo ya shule hiyo alisema kuwa jitihada mbali mbali zimefanyika hasa baada ya shule hiyo kuezuliwa na kimbunga na kuwa jitihada za wadau mbali mbali zimefanyika kukabati vyumba vya madarasa vilivyoezuliwa japo alisema hadi sasa bweni moja bado kukarabatiwa hivyo wanafunzi wanaendelea kulala darasani.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.