Habari za Punde

BAADA YA 'MENGI YASEMWAYO' NGOMA KUTIMKA RASMI YANGA, ALIKUWA AKITIBIWA NA DAKTARI 'FEKI'

Na Mwandishi Wetu, Dar
BAADA ya kuibuka maneno na maswali mengi yasiyokuwa na majibu kuhusu mshambuliaji wa Kimataifa Mzimbabwe wa Yanga, Donald Ngoma, juu ya kinachomfanya kugomea kucheza baadhi ya mechi hususan iliyopita bai yao na Simba, hatimaye Ngoma ameibuka na kuweka wazi kuwa ataondoka katika klabu hiyo ili kukwepa mambo ya hovyo hovyo yanayofanywa na uongozi.
Ngoma amesema hayo wakati akizungumzia tuhuma dhidi yake juu ya kutocheza mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba Jumamosi iliyopita, ambapo Yanga walipoteza mchezo huo kwa kuchapwa mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Mimi na klabu tumefikia katika hatua ambayo nitachukua maamuzi muda si mrefu nitakupa taarifa sahihi za kuondoka kwangu kutokana na mambo ya ovyo ya viongozi wa klabu,” Hii ni kauli yake aliyoandika katika ukurasa wake wa Instagram leo asubuhi.
Aidha, mchezaji huyo amesema kwamba mashabiki na wapenzi wa Yanga wamekuwa wakimshutumu na kumtukana kutokana na taarifa zisizo sahihi 
zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu yeye, 
hali ya kuwa ukweli anao yeye mwenyewe.
“Nimekuwa kimya wakati wote nikitukanwa juu ya sababu za kutocheza, wakati ukweli ni kwamba mimi nina maumivu ya goti. Taarifa nyingi zimekuwa zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba sitaki kucheza kwa sababu ninataka kuondoka katika timu, nashangaa wapi wanapata hizo taarifa,”amesema Ngoma.

Amesema Daktari ambaye Yanga walimtumia kumtibu yeye alikuwa ‘tapeli’ na ameilia fedha klabu bila kufanya kazi yoyote.
“Daktari alikula fedha za viongozi wa klabu na kuwadanganya kwamba alikuwa ananitibu amenipeleka hospitali, wakati ukweli ni kwamba nilikuwa ninatibiwa katika hospitali nyingine kwa gharama zangu mwenyewe,”amesema Ngoma.

Aliendelea kusema kuwa baadaye Daktari huyo alipoulizwa alisema kwamba niko fiti kucheza, wakati ukweli ni kwamba sikuwa tayari kabisa kucheza.
“Alikuwa anawaambia watu kwamba maumivu yangu yanaweza kupona ndani ya wiki mbili, wakati Daktari halisi aliyekuwa ananitibu alisema ninahitaji kati ya wiki sita hadi nane kupona. Tazama huyu Daktari feki alivyoleta mtafaruku kati yangu na timu,”amelalamika Ngoma.
Donald Ngoma anaelekea kukamilisha msimu wake wa pili tangu ajiunge na Yanga akitokea Platinums FC ya Zimbabwe mwaka 2015.
Na amekuwa mchezaji muhimu tangu ajiunge na klabu hiyo yenye maskani yake, Jangwani, Dar es Salaam kiasi kwamba kila alipokosekana pengo lake lilionekana.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.