Habari za Punde

MAMA SAMIA SULUHU MGENI RASMI UKARIBISHO WA VIONGOZI DODOMA.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewasili mkoani Dodoma, Makao Makuu ya nchi na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Jordan Rugimbana pamoja na viongozi wengine ambapo kesho atakuwa mgeni Rasmi kwenye Hafla Maalum ya kuwakaribisha Mawaziri, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara pamoja na watumishi wote wa umma waliohamia Makao Makuu Dodoma wakitokea Dar es Salaam kama sehemu ya utekelezaji wa agizo la Mhe Rais na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi .
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na mwenyeji wake,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Jordan Rugimbana
**********************************************
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla maalumu ya kuwakaribisha viongozi wa Serikali itakayofanyika Machi 5 mwaka huu mkoani Dodoma.
Hafla hiyo imeandaliwa na Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Dodoma na itafanyika mkoani humo katika viwanja vya Nyerere (Nyerere Square) kuanzia saa 8 kamili mchana.
Afisa Habari wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, Jeremia Mwakyoma ameyasema hayo leo mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya ujio wa viongozi hao katika Mkoa huo.
Mwakyoma amesema viongozi wa Serikali kuhamia katika Makao Makuu ya Nchi ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano hivyo Mkoa utawakaribisha rasmi Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara waliohamia kutoka Jijini Dar es Salaam.
“Tukio la viongozi wa Wizara kuhamia Makao Makuu Dodoma ni la kihistoria ndio maana uongozi wa Serikali ya Mkoa umeona ni vema kuweka utaratibu rasmi wa kuwakaribisha viongozi hao,”alisema Mwakyoma.
Afisa Habari Mwakyoma amewakaribisha wananchi wote wa Mkoa huo pamoja na Mikoa ya jirani kuhudhuria kwa wingi kwenye hafla hiyo.Mnamo Julai 25 mwaka 2016 katika maadhimisho ya siku ya mashujaa yalioadhimishwa mkoani Dodoma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli alitangaza rasmi Serikali kuanza mchakato wa kuhamia Dodoma ambapo ndipo yalipo Makao Makuu ya Nchi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.