Habari za Punde

TANZANIA KUPELEKA MADAKTARI 500 KUAJILIWA NCHINI KENYA

 Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto imebainisha kuwa inatarajia kuwapeleka Madaktari wake waliopo nchini Tanzania kwenda kufanya kazi nchini Kenya kufuatia kuombwa na Rais wa nchi hiyo Mhe. Uhuru Kenyatta.
Akizungumza na vyombo vya habari mapema leo, Waziri wa Afya, Mh. Ummy Mwalimu amesema kuwa, ujumbe maalum kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta kupitia kwa Wiziri wake wa Afya uliokutana na Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli  na kuomba ombi lao hilo la kutaka madaktari 500, ambao wataajiliwa kwa mikataba maalum ya kuanzia miaka 2 kwa kufanya kazi nchini Kenya.
“Natoa rai kwa madaktari wazawa waliopo nchini kuomba nafasi za ajira ya Udaktari  nchini Kenya kwa mkataba maalum. Zoezi hilo limeanza rasmi leo Machi 18 mpaka Machi 27, mwaka huu wawe wameomba.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa waombaji ni wale watakaokidhi vigezo maalum ikiwemo asiwe katika utumishi wa Umma, Asiwe amejiliwa na mashirika ya umma ama mashirika teule ambayo yanalipiwa na Serikali.
Kwa Mujibu wa Waziri Ummy ameeleza kuwa muombaji lazima awe amehitimu mafunzo ya “internalship” na mwisho awe amesajiliwa na baraza la Madaktari  nchini.
Aidha, Waziri Ummy ameweka wazi kuwa, ajira hiyo itakuwa ni ya miaka miwili ambapo watapata mishahara na malupulupu mbalimbali katika ajira zao hizo huku akibainisha kuwa, jambo hilo ni jema na linaiingizia Taifa sifa kwa kupeleka wataalamu wake nje ya nchi kupata ajira.
Kwa upande Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Mpoki Ulisubisya amesema kuwa, moja ya vigezo ambavyo vinahitajika kwa madaktari hao ni pamoja na kuwa na digrii ya kwanza na Internal ship huku akiongeza kuwa, kwa upande wao Wizara imejipanga kuimalisha madaktari wa ndani ikiwemo kiwaajili.
Naye Katibu Mkuu Utumishi, Mh. Laulian Ndumbalo amewatoa hofu watanzania licha ya kuwapeleka Madaktari hao nje kupatiwa ajira, nchini bado ina Madaktari wengi wanaofikia zaidi ya 1000, huku kila mwaka wakiajili Madaktari 400 hadi 450.
Imeelezwa kuwa  Madaktari hao watakaojitokeza watapata faida kubwa kwani watakuza mahusiano mema ya nchi za Afrika Mashariki kupitia kada hiyo huku pia wakitarajia kuipatia maendeleo nchi ya Tanzania. Jambo ili ndio la kwanza linafanyika huku ikielezwa kuwa idadi hiyo ya madaktari kutoka Tanzania kwenda kupatiwa ajira nje ya mipaka yake ni kubwa, licha ya madaktari wengi kuwepo nchi mbalimbali ikiwemo Malawi, Zambia, Afrika Kusini, Botswana na mataifa mengine.
Madaktari hao wenye kutaka kujiunga wanaweza kutembelea tovuti ya wizara ya Afya na kupata maelezo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.