Habari za Punde

WANAWAKE WATAKIWA KUWASHIRIKISHA WANAUME KUTATUA BAADHI YA CHANGAMOTO

Na: Jovina Bujulu – MAELEZO
Mizigo mikubwa waliyonayo wanawake ni miongoni mwa changamoto za kijamii ambazo zimekuwa kikwazo kwa wao kushiriki kikamilifu katika masuala ya siasa.
Hayo yamesemwa na Balozi Getrude Mongella ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Bunge la Afrika alipokuwa akizungumzia ushiriki wa wanawake katika siasa nchini.
“Changamoto kubwa ni pamoja na teknolojia duni ambayo inamlazimisha mwanamke kuendelea kulima kwa kutumia jembe la mkono, kutembea umbali mrefu kutafuta maji, kutafuta kuni na suala zima la kulea watoto” alisema Balozi Mongella.
Akizungumzia suala la teknolojia duni alisema kuwa katika nchi zinazoendelea hilo limeendelea kuwa tatizo kubwa na kwa kuwa wanawake ndio wazalishaji mali wakubwa, wamejikuta wanaweka nguvu zao nyingi katika matumizi ya jembe la mkono. Hivyo ukulima kwa kutumia jembe la mkono haukidhi mahitaji yao ya chakula katika familia na kujikuta wamebaki kuwa omba omba.

Pamoja na changamoto hizo Balozi Mongella amesema kuwa ushiriki wa wanawake bado ni mkubwa na ameitaka jamii kuwawezesha kubeba baadhi ya mizigo kwa mfano kuimarisha huduma za afya ya jamii.
Balozi Mongella alitoa ushauri kwa jamii kutokukaa kimya bali kuzungumzia changamoto hizo na utatuzi wake ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wanaume, kwani wakielimika na kutumika vizuri baadhi ya changamoto zitaondoka na kasi ya mwanamke kupiga hatua itakuwa kubwa.
Aidha, alivitaka vyama vya wanawake kuamka na kuendeleza mapambano ya kumkomboa mwanamke kwani ajenda ya wanawake  ni ya kudumu na haijakamilika hata kidogo.
Zaidi ya hayo, Balozi Mongella amewataka wanawake kutambua nafasi yao katika kuchangia uchumi wa taifa, ili wafike mahali waonyeshe mchango wao katika Tanzania ya viwanda ambayo Watanzania wanaitaka na kuwashauri wanawake waliopata elimu kusaidia kuwavusha wanawake wengine.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo ambaye alikuwa Mgombea Urais pekee mwanamke katika uchaguzi uliopita wa 2015, Mama Anna Mgwira alisema wanawake wakipewa nafasi wanajitoa kwa ukamilifu hivyo aliwataka wasimamie nafasi zao huku wakifanya kazi kwa weledi, uaminifu, wajiheshimu na wawajibike ili kuondokana na dhana ya kwamba hawawezi kazi bila kusimamiwa na kusaidiwa

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.