Habari za Punde

WASANII MSIVUKE MIPAKA KATIKA UTENGENEZAJI WA KAZI ZENU KWA KUVUNJA SHERIA ZA NCHI: DKT. MWAKYEMBE

 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) mara baada ya kumaliza mazungumzo na Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego Ofisini kwake Mjini Dodoma.
Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) mara baada ya kumaliza mazungumzo na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe Mjini Dodoma. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe akisalimiana na Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego kwa mwaliko Ofisini kwake Mjini Dodoma kufanya mazungumzo yahusuyo mambo ya Sanaa ya Muziki.
  Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego akitia saini katika kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe Mjini Dodoma kwa mazungumzo.
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe akimsisitiza jambo, Msanii wa Muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego mara baada ya mazungumzo Ofisini kwake Mjini Dodoma.
 Picha zote na Raymond Mushumbusi WHUSM Dodoma
*******************************************
Na Raymond Mushumbusi WHUSM Dodoma
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe ametoa wito kwa wasanii nchini kutovuka mipaka katika utengenezaji wa kazi zao mpaka kufikia hatua ya kuvunja Sheria na taratibu za nchi.
Ameyasema hayo Mjini Dodoma jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukutana  na kufanya mazungumzo na Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego kwa mwaliko wa Waziri huyo.
Amesema kuwa  wasanii ni nguzo muhimu katika nchi sio kwa kufanya kazi ya  kuburudisha na kuelimisha bali katika kuujenga Utamaduni wa nchi ambao ndio nguzo muhimu sana kwa malezi na makuzi ya wanajamii.
“Niwaombe wasanii nchini kuzingatia Sheria na taratibu za nchi katika utunzi wao na utenegenezaji wao wa kazi zao” Alisisitiza Mhe. Dkt Mwakyembe.
Aidha ameongeza kuwa Serikali haina nia ya kuwanyima uhuru wa kujieleza bali watambue kuwa nchi inaendeshwa kwa taratibu na Sheria ambazo zinatakiwa zifuatwe na watu wote.
Kwa upande wake Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli  kwa kuwaunga mkono wasanii nchini na kuahidi kuongeza baadhi ya mambo katika wimbo wake wa “Wapo” na kuwaalika watanzania kama kuna kero zingine zinazowasumbua katika jamii wasiwasilishe kwake ili azizungumzie katika wimbo huo.
“Namshukuru Mhe. Rais kwa kutuunga mkono pia naahidi kufanya “remix” ya wimbo wa “Wapo” kwa kuongeza maneno niliyoshauriwa na Mhe Rais na Mhe. Waziri na kama kuna mengine kutoka kwa wananchi pia niko tayari kuyapokea na kuyafanyia kazi” alisema Bw. Elibariki. 
Hivi karibuni wimbo wa “Wapo” wa Msanii Emmanuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitego ulifungiwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kosa la kutozingatia maadili na baadae kufunguliwa kwa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli  kupitia Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.