Habari za Punde

YANGA YAPANGWA KUANZA NA WAARABU KOMBE LA SHIRIKISHO

BAADA ya Yanga kutolewa na Zanaco katika michuano ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika, na kuangukia katika michuano ya kombe la Shirikisho, sasa imepangiwa kukipiga na timu ya Mouloudia Club d'Alger, maarufu kama MC Alger ya Algeria katika mchujo wa kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya droo iliyopangwa mchana huu mjini Cairo, Misri yalipo makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Akizungumza na mtandao huu Kocha msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi, alisema kuwa alilijua hilo kuwa watapangiwa kuanza mchezo wao wa kwanza nyumbani, na kumalizia ugenini kutokana na kwamba ni kasumba waliyojijengea timu nyingi za kiarabu.
''Kwa hili la kuanzia nyumbani na kumalizia ugenini nililijua tu kwani waarabu ni kawaida yao ili wao wamalizie nyumbani, lakini hilo halina shida tunajiandaa kukabiliana na lolote litakalojitokeza mbele yetu, ilimradi kuvua hatua ya mtoano''. alisema Mwambusi.
Katika hatua hiyo iwapo Yanga watafanikiwa kuwagalagaza Algas wataingia hatua ya makundi, huku mchezo wa kwanza utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jiji Dar es Salaam, ukitazamiwa kupigwa kati ya Aprili 7, 8 hadi 9 mwaka huu.
Droo hiyo imehusisha timu zilizovuka hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho dhidi ya zilizotolewa kwenye hatua hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu zilizotolewa Ligi ya Mabingwa zitamenyana na zilizosonga mbele Kombe la Shirikisho katika mechi za nyumbani na ugenini kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.