Habari za Punde

YANGA YAVUNJA MKATABA NA MKURUGENZI WAKE PLUIJM

KLABU ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, leo imemkabidhi rasmi barua ya kuvunja mkataba Mkurugenzi wake wa benchi la Ufundi, aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hans Van De Pluijm.
Pamoja na Katibu Mkuu wa timu hiyo, Boniface Mkwasa, kukataa kuweka wazi juu ya suala hilo, lakini Mholanzi huyo amesikika akihojiwa na Kituo kimoja cha redio na kukili kupokea barua hiyo, ambapo Uongozi umesema kuwa utatoa taarifa rasmi.
Aidha imeelezwa kuwa Yanga wameamua kuvunja mkataba na Pluijm kwa kile kilichoelezwa ukata wa kifedha unaoikabili Klabu hiyo kwa sasa.
“Leo niliitwa na Katibu (Charles Boniface Mkwasa) akaniambia kutokana na hali mbaya ya kifedha ya klabu kwa sasa, hawawezi kuendelea na mimi. Akanipa barua ya kunivunjia mkataba, nikaondoka zangu,”alisema Van 
Mpaka anakabidhiwa barua hiyo hii leo, Pluijm anaidai Yanga mishahara ya miezi kadhaa na kutokana na kumvunjia mkataba klabu hiyo inapaswa kumlipa. “Hakuna wasiwasi, nitakaa nao na kuzungumza nao namna ya kulipana,”alisema.
Hata hivyo, Pluijm alisema anasikitika klabu imefanya maamuzi bila kumshirikisha, kwani naye alikuwa tayari kuvumilia hali ngumu ya sasa. “Nimekuwa Yanga katika wakati mzuri, na hili lililotokea sasa kila mtu anajua, nami nilikuwa tayari kuvumilia, ila wamefanya maamuzi bila kunishirikisha,”alisema.  
Pluijm amesema anaondoka Yanga, lakini anataka ieleweke klabu hiyo ipo ndani ya moyo wake na atakuwa tayari siku moja kurejea tena akihitajika.
Yanga ilimhamishia Pluijm kwenye Ukurugenzi wa Ufundi Novemba mwaka jana, baada ya kumleta Mzambia, George Lwandamina awe kocha Mkuu.
Pluijm amefundisha Yanga kwa awamu mbili tangu mwaka 2014 alipoanza kwa kufanya kazi kwa nusu msimu, akimpokea Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts kabla ya kwenda Uarabuni.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.