Habari za Punde

KAGERA SUGAR YAWAKATIA UMEME SIMBA MBIO ZA UBINGWA YAIDUWAZA 2-1

Kikosi cha Kagera Sugar: Juma Kaseja, Godfrey Taita, Mwaita Gereza, Juma Shemvuni, Mohamed Fakhi, George Kavila, Suleiman Mangoma, Ame Ally ‘Zungu’/Ally Ramadhani, Edward Christopher/Themi Felix, Mbaraka Yusuph na Japhet Makalai/Anthony Matogolo.
Kikosi cha Simba SC: Daniel Agyei, Muzamil Yassin, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla/Juma Luizio, Laudit Mavuo, Ibrahim Hajib/Mohammed Ibrahim na James Kotei
*********************************************
TIMU ya Kagera Sugar leo imewaduwaza mashabiki lukuki waliofika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba baada ya 'kukata umeme' na kuwabakiza Simba katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa leo jioni, huku Simba wakikubali kichapo cha mabao 2-1.
Baada ya watani zao Yanga jana kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam Fc na kukaa kileleni mwa ligi hiyo, wakiwa na Pointi 56, Simba wao kwa kichapo hicho wameendelea kubaki nyuma ya watani zao wakiwa na Pointi zile zile 55.
Katika mchezo huo uliochezeshwa Jimmy Fanuel, aliyesaidiwa na Joseph Masija wa Mwanza na Geoffrey Msakila wa Geita,hadi mapumziko Kagera Sugar walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji chipukizi, Mbaraka Yussuf Abeid, katika   dakika ya 27 kwa shuti kali la umbali wa mita 22 baada ya pasi ya mchezaji mwenzake wa zamani wa Simba B, Edward Christopher.
Kipindi cha pili, Kagera Sugar walitangulia tena kupata bao kupitia kwa Edward Christopher aliyemalizia pasi ya Sulemani Mangoma dakika ya 47 kabla ya Muzamil Yassin kuifungia Simba bao la kufutia machozi katika dakika ya 67 akimalizia pasi ya James Kotei.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.