Habari za Punde

KAMATI SHERIA NA HADHI ZA WACHEZAJI YAAHIRISHA KIKAO KUENDELEA TENA KESHO

Na Asia Gamba, Dar
KIKAO cha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya sakata la beki Mohammed Fakhi kuichezea Kagera Sugar dhidi ya timu yake ya zamani, Simba akiwa ana kadi tatu za njano kimeahirishwa hadi kesho.
Kikao hicho kilichoanza Saa 4:00 asubuhi katika hoteli ya Protea, Masaki, Dar es Salaam kimefungwa Saa 2:05 usiku na Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa akasema kitaendelea kesho, jumatano 
Mwesigwa amesema wanahitaji vielelezo na ushahidi zaidi ili kujiridhisha kabla ya kutoa maamuzi na zoezi hilo litaendelea kesho.
Utata upo katika mchezo wa Jumatano ya Januari 18, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kati ya wenyeji Kagera Sugar na African Lyon ya Dar es Salaam, ambao inadaiwa Fakhi alionyeshwa kadi ya njano wakati klabu yake inapinga.
Viongozi wa klabu za Simba, African Lyon, Kagera Sugar, marefa na Fakhi mwenyewe walihojiwa leo Protea kwa nyakazi tofauti na taarifa zinakinzana.
Baadhi ya waliohojiwa wanasema kweli Fakhi alikuwa ana kadi tatu, lakini wengine wamesema mchezaji huyo hakuwa na kadi tatu.
Kikao hicho kinafuatia Kagera Sugar kupinga uamuzi wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kuipa Simba SC pointi tatu na mabao matatu kutokana na Rufaa waliyoikatia timu hiyo kwa madai ya kumtumia Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo Aprili 2, mwaka huu.
Katika barua iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Kagera Sugar, Hamisi Madaki kuelekea kwa Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa, klabu hiyo imeliomba shirikisho hilo kupitia upya maamuzi ya Kamati ya Saa 72 kwa kuwa Fakhi hakuwa na kadi tatu za njano kama ilivyodaiwa.
 Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na Kagera Sugar kumchezesha Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.