Habari za Punde

KOCHA WA KIMATAIFA WA KUOGELEA KUSHUHUDIA MASHINDANO YA TAIFA

  Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar
Kinyang’anyiro cha kuwatafuta waogeleaji bora wa Tanzania kwa ajili ya timu mbalimbali za Taifa kitaanza kesho kwenye bwawa la kuogelea la Hopac ambapo jumla ya waogeleaji 172 watawania nafasi hiyo.
Mbali ya kuwania nafasi hiyo, waogeleaji hao pia watapata fursa ya kuonyesha vipaji vyao kwa kocha maarufu wa mchezo huo kutoka  Uingereza, Sue Purchase ambaye anatafuta wachezaji nyota kwa ajili ya kujiunga na shule yake ya St Felix ambayo inatamba kwa mchezo huo nchini Uingereza.
Purchase amewasili jijini tayari na pia atatembelea klabu ya Dar Swim Club (DSC) na kufanya mazungumzo ya wazazi, waogeleaji na makocha wa klabu hiyo maarufu jijini.
Purchase ambaye pia  ni mkurugenzi wa mchezo wa kuogelea wa shule hiyo, ameamua kuja nchini baada ya kuvutiwa na vipaji vya waogeleaji watano wa Tanzania wanaosoma kwa njia ya ‘scholarship’ maalum nchini Uingereza kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa  Chama cha Kuogelea (TSA), Ramadhani Namkoveka.
Waogeaji  wa Tanzania wanaosoma nchini Uingereza ni Tumiotto, Collins Saliboko, Anjani Taylor,  Smriti Gokarn na Aliasgar Karimjee.
Namkoveka amesema kuwa wameandaa mashindano mazuri kutokana na udhamini wa Davis & Shirtliff, CRDB Bank, Mediterraneo Hotel & Restaurant, Coca Cola, Aggrey & Clifford na The Terrace.
“Ni faraja kubwa sana kupata ujio huu, Purchase ni kocha maarufu na mwenye heshima kubwa nchini Uingereza, amesaidia waogeleaji wengi sana ambao kwa sasa ni nyota katika mchezo huo duniani,” alisema Namkoveka.
Alisema kuwa mbali ya kushuhudia mashindano hayo na kusaka vipaji, kocha huyo atakutana pia na wazazi na, makocha, waogeleaji wa klabu ya Dar Swim Club na kufanya  nao mazungumzo.
“Pia atafanya mazungumzo na makocha na wadau wote wa mchezo wa kuogelea siku ya Jumapili kuanzia saa 4.00 asubuhi kwenye ukumbi wa Slipway, hivyo tunawaomba makocha na wadau kufika kwa wingi, siku hiyo pia atatoa tathmini ya mashindano ya Taifa baada ya kuhudhuria,” alisema.
Alisema kuwa hii ni faraja kwa wadau, wachezaji, vilabu  na viongozi wa mchezo wa kuogelea kwani ujio wa kocha huyo ni ishara ya mchezo kukua.
Mashindano hayo yatashirikisha jumla ya klabu 15 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambazo zitashindana katika staili za backstroke, freestyle, breaststrokes, Butterfly na Individual Medley (IM).

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.