Habari za Punde

MAAMUZI YA KIKAO CHA KAMATI YA SAA 72, BANDA 'JELA' KWA UBONDIA


KAMATI ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania au Kamati ya Saa 72, ilifanya kikao chake juzi Ijumaa Aprili 7, 2017 jijini Dar es Salaam na kufikia uamuzi ufuatao.

Kuhusu kupulizwa dawa vyumbani Uwanja wa Kambarage

Daktari wa Uwanja wa Kambarage, Dk. Abel Kimuntu amekataa kuwasilisha taarifa yake kuhusu tuhuma za kupuliziwa dawa kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha timu ya Majimaji katika mechi namba 170 ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya wenyeji Stand United. Klabu ya Majimaji iliwasilisha malalamiko yake kwa Bodi ya Ligi kuhusu suala hilo.

Hivyo, Kamati imeagiza suala la daktari huyo lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya hatua za kinidhamu dhidi yake kutokana na kukataa kutoa ushirikiano kwa mwendeshaji wa Ligi juu ya jambo hilo. Kamati ya Nidhamu inatarajiwa kukaa wakati wowote wiki ijayo.

Kuhusu Mchezaji Abdi Banda

Mechi namba 194 (Kagera Sugar 2 vs Simba 1). Beki wa Simba, Abdi Banda jezi namba 24 amesimamishwa kucheza Ligi Kuu wakati akisubiri suala lake la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla jezi namba 15 wakati akiwa hana mpira kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Alifanya kitendo hicho ambacho hakikuonwa na waamuzi katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 2, 2017 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Uamuzi wa Kamati umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu.
Pia Kamati ilibaini kuwa Banda alifanya kitendo cha aina hiyo kwenye mechi namba 169 kati ya Simba na Yanga iliyofanyika Februari 25, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali, Klabu ya Kagera Sugar iliwasilisha malalamiko dhidi ya kitendo cha beki wa Simba, Abdi Banda kumpiga ngumi kiungo wao George Kavilla wakati akiwa hana mpira, na Mwamuzi wa mechi hiyo kutochukua hatua yoyote.Kwa vile kosa hilo ni la kinidhamu, Kamati imemsimamisha Abdi Banda kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) wakati akisubiri suala lake kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Kamati ya Nidhamu inatarajiwa kukaa wakati wowote wiki ijayo.
Kadhalika Klabu ya Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na timu ya Kagera Sugar kumchezesha mchezaji Mohamed Fakhi Gharib wakati akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.Kamati baada ya kupitia malalamiko hayo, imeahirisha shauri hilo hadi Alhamisi Aprili 13, 2017 kwa vile bado inafuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu malalamiko hayo kabla ya kufanya uamuzi.
Mechi namba 195 (Yanga 1 vs Azam 0). Yanga haikuingia kwenye chumba chake cha kubadilishia nguo, kutokana na kuwa na maji yaliyomwagwa na wanachama wa klabu hiyo (makomandoo) muda mfupi kabla ya timu hiyo kuwasili uwanjani.
Kamati imeelekeza klabu ya Yanga iandikiwe barua ya onyo, na kuitaka kuhakikisha wanachama wake wanaacha mara moja mtindo wa kumwaga maji vyumbani baada ya kuwa vimeshafanyiwa usafi na wafanyakazi wa uwanja tayari kwa ajili ya matumizi ya timu yao.
Mechi namba 200 (Majimaji 4 vs Toto Africans 1). 
Katika mechi hiyo, timu ya Toto Africans ilifanyiwa vurugu ikiwa njiani kurejea hotelini baada ya mechi hiyo ambapo viongozi wake wawili waliumizwa. Tukio hilo liliripotiwa Kituo cha Polisi, na kesi tayari iko kortini.
Kituo cha Songea (Uwanja wa Majimaji) kiandikiwe barua ya kuhakikisha hazitokei vurugu uwanjani hapo baada ya mechi ikiwemo kuhakikisha timu ngeni inatoka uwanjani salama hadi kwenye hoteli ilikofikia. Iwapo vurugu zitaendelea, Bodi ya Ligi itasimamisha matumizi ya kituo hicho kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 9(2) ya Ligi Kuu.

KUPITIA MATUKIO YA LIGI DARAJA LA PILI (SDL Play Off)
Mechi namba 7 (Mawenzi Market 2 vs Transit Camp 0). Klabu ya Transit Camp imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) baada ya timu yake kuchelewa uwanjani kwa dakika 45 katika mechi hiyo iliyochezwa Machi 18, 2017 katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Adhabu dhidi ya Transit Camp imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(1) na 14(47) kuhusu Taratibu za Mchezo.

Kocha Msaidizi wa Transit Camp, Thomas Gama amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kutolewa nje na Mwamuzi katika mchezo kutokana na kumtolea maneno ya kashfa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja.
Mechi namba 8 (JKT Oljoro 1 vs Cosmopolitan 0). Klabu ya Cosmopolitan iliwasilisha malalamiko kuwa mechi hiyo iliyofanyika Machi 20,2017 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha ilichezeshwa na Mwamuzi wa Arusha, badala ya Mwamuzi kutoka Singida aliyekuwa amepangwa awali.
Kamati imetupa malalamiko hayo kwa vile si ya kweli, na Mwamuzi aliyechezesha mechi hiyo alitoka Mkoa wa Manyara, na si Arusha kama walivyodai katika malalamiko yao.
Mechi namba 12 (Transit Camp 1 vs Cosmopolitan 1). Daktari wa Cosmopolitan, Najim Mtoro amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kumtukana Mwamuzi wa Akiba.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.