Habari za Punde

RAIS MAGUFULI KUZINDUA UJENZI WA RELI YA TRENI YA UMEME DAR-MORO KESHO

*Kasi yake ni  kilomita 160 kwa saa
* Inakwenda kasi sawa na ndege ndogo angani
*Dar – Moro saa 1:16
*Dar - Dodoma  saa 2:30
*Dar -Mwanza  saa 7:30.
***************************************************************
Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar
RAIS  Dkt. John Magufuli,  anatarajia kuzindua rasmi  mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya Treni ya umeme kesho‘ standard gauge’  itakayofanya safari zake kati ya mkoa wa Dar es Salaam na Morogoro.
Hafla ya uzinduzi huo itafanyika katika eneo la Pugu, Wilaya ya Ilala,  jijini Dar es Salaam,  ambapo pamoja na kukagua mradi huo, Rais ataweka jiwe la msingi la uzinduzi wa ujenzi huo. .
Kipande  cha reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kitakuwa na urefu wa Kilomita 300 na ujenzi huo ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi mzima wa reli hiyo  inayotarajiwa kuanzia Dar es Salaam kupitia Pwani, Morogoro, Dodoma, Tabora, Isaka hadi Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wananchi,baada ya kutembelea eneo la mradi huo, Pugu, Kiongozi aliyetembelea kukagua maandalizi ya uzinduzi huo, alisema, uzinduzi wa mradi huo utaandika historia mpya ndani ya taifa la Tanzania.
 “Hii ni siku nyingine ambayo Mungu ametupa kibari  kwa mkoa wetu na kwa taifa letu kwa ujumla, ambapo Rais Dk. Magufuli  anakwenda kutimiza ndoto yake na azma yake ya kuandika  historia ya kwanza katika taifa letu ya kutujengea reli yenye viwango vya juu vya kimataifa,”alisema 
Aidha alisema treli itakayokuwa inapita katika reli hiyo itamwezesha mwananchi kusafiri na kusafirisha mizigo kwa haraka  hivyo itasaidia kuchochea maendeleo.
“Fahari kama hii,  uwezo na mapenzi makubwa  ambayo Rais Dk. Magufuli anayo,  sisi ni  lazima tumjibu kwa kufanya kazi kwa bidii.  Natoa rai kwa wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam, kujitokeza kwa wingi  kushiriki hafla ya uzinduzi huu hapo kesho,” alisema 
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Hodhi Miliki ya  Rasilimali za  Reli Tanzania (RAHCO) Mhandisi Masanja Kadogosa, alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro itakuwa na urefu wa Kilomita 205.
“Lakini kipande kingine ni cha urefu wa Km 95 ambacho  ni kwa ajili ya treni kugeuza hivyo kufikisha jumla ya Kilomita 300,”alisema Kadogosa.
 Kadogosa alisema kuwa ujenzi wa reli hiyo utachukua muda wa miezi 30 kuanzia sasa  na kuhusisha ujenzi wa miundombinu ya umeme, Stesheni sita za abiria na sita za kupishani treni na ujenzi wa wigo wa Kilomita 102 kwa usalama wa watu na magari.
Alisema  hiyo ni awamu ya kwanza ya ujenzi ambapo awamu ya pili itaendelea  kati ya mkoa wa Morogoro hadi Dodoma, kisha Tabora, Isaka na Mwanza.
Kadogosa alisema treni ya umeme itakayo pita katika reli hiyo itatumia muda wa  saa 2:30 tu kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

Kuhusu suala la ajira wakati  wa ujenzi wa reli hiyo, Kadogosa aliwatoa hofu wananchi waliofurika  katika eneo la  mradi Pugu kwamba vibarua na wafanya kazi watachukuliwa kwa utaratibu maalum.
Mataperi wa wawaliza vijana wanaosaka ajira
Baadhi ya  wananchi wanao saka ajira na vibarua katika mradi huo walipaza sauti zao kwamba  kuna baadhi ya watu wamejitokeza na kuchukua fedha  kuanzia sh.1000 hadi 100,000 wakiahidi kuwatafutia nafasi katika mradi huo.
“Wanakusanya fedha  zetu lakini ajira zenyewe hatupewi . Tusaidieni,” alipaza sauti  kijana mmoja mbele ya  viongozi.
Kijana mwingine alisema watu wanaokusanya fedha zao wanajitambulisha kwamba wanahusika na mradi huo.
Kutokana  na hali hiyo ilimlazimu  Mhandisi Kadogosa kutoa onyo  kali kwa wananchi hao kutokuthubutu kutoa fedha kwa ahadi ya kupewa vibarua au ajira katika mradi huo na kwamba kutoa fedha ni kutoa rushwa.
“Ukitoa fedha ili upate ajira au kibarua  ni sawa na kutoa rushwa. Msitoe rushwa.Baada ya uzinduzi hu kuna utaratibu wa ajira utatangazwa. Tutawaajiri  watu wengi  hapa. Msitoe fedha kwa watu msio wafahamu. Wanawaongopea,”alisema Kadogosa hali iliyorudisha matumaini ya wananchi hao.
Tujikumbushe kuhusu mradi
Januari mwaka huu Serikali ilitiliana saini  makubaliano ya ujenzi wa sehemu ya kipande  hicho cha reli ya kampuni za Yapi Merkezi ya uturuki na Mota-Engil  Africa   ya Ureno kwa grahama ya dola zaidi ya bilioni moja za kimarekani sawa na zaidi ya  sh. trilioni mbili.
Akishuhudia utiliaji saini  huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, alisema, treni hiyo itakwenda kwa  kasi ya kilometa 160 kwa saa na  itakuwa ni ya kwanza kwa Afrika ikifuatiwa na nchi ya Morocco.
“Tunataka kuifanya nchi yetu iwe ndogo kwa kutumia miundombinu ya kisasa ndio maana serikali imeamua kujenga reli hii itakayotumia umeme na kwenda kwa kasi  kubwa kuliko nyingine zote barani Afrika”, alisema  Profes Mbarawa.
Muda
Treni hiyo itakayotumia reli hihiyo itakuwa ikitumia muda mfupi  ambapo sari ya Dar es  Salaam hadi Morogoro  itatumia muda wa saa 1:16 wakati Dar es Salaam  hadi Dodoma itatumia muda wa saa 2:30 na safari ya Dar es Salaam hadi Mwanza itatumia muda wa saa 7:30.
Aidha, Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa gharama za ujenzi wa reli hiyo haitakuwa sawa na mikoa mingine kutokana na kutofautiana na hali ya jiografiia kwenye mikoa ambapo reli hiyo itapita.
Ujenzi utakaofuata
Kwa mujibu wa taarifa ya awali ya Waziri  Mbarawa baada kukamilika kwa  awamu hiyo ya  kwanza ya  ujenzi  awamu nyingine  zitakazofuata ni kutoka Morogoro hadi Makotopora (Kilomita  336), Makotopora hadi Tabora (Kilomita  294), Tabora hadi Isaka Kilomota 133 na Isaka hadi Mwanza Kilomita ( 248) .

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.