Habari za Punde

SERIAKLI YATENGA MAENEO YA UWEKEZAJI MKUBWA MJINI DODOMA

Na Judith Mhina - MAELEZO
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetenga maeneo ya uwekezaji mjini Dodoma kwa ajili ya kujenga viwanda, mahoteli makubwa, nyumba za makazi na huduma muhimu za kijamii.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) Mhandisi Paskas Muragili amesema kuwa maeneo hayo ni Njedengwa, hekta 580 ambapo miundombinu muhimu imewekwa ikiwemo maji, umeme na barabara ya lami ili kurahisisha uwekezaji, eneo la Iyumbu hekta 78 na Western Industrial Area hekta 334.6 (WIA). 
Mhandisi Muragili ameongeza CDA imetenga hekta 14,700 eneo la Kikombo, Chigongwe hekta 6, 278, Nyankali hekta 2,495 na Mtumba hekta 8,000, kwa ajili ya kujenga mji wa Serikali ambapo kutajengwa Wizara mbalimbali, Idara za Serikali, Taasisi, na mashirika yatakayowekeza Dodoma.
Vilevile, eneo hilo litajengwa makazi ya watumishi wa Umma na huduma mbalimbali za kijamii kama masoko, zahanati, hoteli, maduka na nyumba za kuabudia kulingana na imani zao. 
Akikaribisha wawekezaji kuwekeza Dodoma, Muragili amewahasisha Watanzania na wasio watanzania kuchangamkia fursa hiyo kwa kujenga hoteli za kitalii za nyota tano na zile za kawaida, kwa kuwa mji unategemea kupata wageni wengi siku za usoni. 
“Nawakaribisha wawekezaji wa ujenzi wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo, bila wasiwasi niwahakikishie ardhi iliyopo Dodoma inatosha kwa uzalishaji mkubwa wa malighafi mbalimbali zitakazohitajika viwandani”. 
“Aidha, Mkoa huu upo katikati ya Tanzania hivyo malighafi yoyote itakayohitajika ni rahisi kufika Dodoma ambayo imeunganishwa kila kona na barabara za lami,” alisema Muragili.
Pia mikoa inayoizunguka Dodoma ikiwemo Manyara, Singida, Iringa na Morogoro inaweza kunufaika kwa wepesi zaidi na fursa hizo.
Akiwatoa hofu wakazi wa Dodoma Muragili amesema; “Ardhi itauzwa kwa bei ya kawaida ili wananchi waweze kumiliki viwanja”. 
Ameyasema hayo akijibu hoja za waandishi wa habari kuhusu kauli za wananchi kudai bei ya viwanja itapanda, kutokana na ujio wa Makao Makuu ya Serikali, ambapo wananchi wa kipato cha chini hawataweza kumiliki viwanja hivyo. 
Muragili alisisitiza kuwa viwanja havitapandishwa bei kwani kwa sasa CDA inauza mita moja ya mraba ya kiwanja cha makazi Shilingi 5,500 hadi 10,000 za fedha ya Tanzania, katika maeneo ambayo kitaalamu tunayaita “medium density”. 
Aidha, alisema kuwa viwanja kwa ajili ya uwekezaji mkubwa mita moja ya mraba ni Shilingi 13,300 fedha ya Tanzania, maeneo hayo kitaalamu yanaitwa “low density”. 
Mhandisi Paskasi Muragili ametoa angalizo kwa wanaohitaji kununua viwanja mjini Dodoma ya kwamba anayetaka kiwanja lazima afike na kufuata taratibu za ofisi za CDA kwa kuwa ndiko viwanja vinakopatikana. “
“Tusinunue viwanja kienyeji, mwisho wa yote utakuwa umedanganywa na madalali ambao kisheria ardhi ya mji wa Dodoma iko chini ya CDA na haihitaji dalali ila ufuate taratibu zilizowekwa”, alisema Muragiri.
Alimalizia kwa kusema “Kwa wale wanaohitaji ardhi nje ya Dodoma kama Mpwapwa, Kongwa, Bahi, Kondoa, Chemba na Chamwino wahakikishe wanawasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ili wapate taratibu rasmi za ununuzi wa ardhi.
Mapaka sasa eneo la WIA lina viwanda kama Machinjio ya kisasa Dodoma na viwanda vya magodoro QFL na Dodoma Halisi.
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ni miongoni mwa Mamlaka zilizopata ufadhili wa kutekeleza mradi wa Uboreshaji Miji Kimkakati unaofadhiliwa na Mkopo wa Benki ya Dunia na msaada kutoka Serikali ya Denmark. 
Aidha, tamko la serikali la mwaka 1973 lenye tangazo namba 230 la tarehe 12 Oktoba 1973 ndio liilianzisha Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma kama mji mkuu wa Serikali ulipewa majukumu makuu 8. 
Kutokana na wimbi la mataifa ya Afrika kubadili miji mikuu, liliingia pia hapa nchini, na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa kwanza wa Tanzania, ambaye ni miongoni mwa wana watiifu wa Afrika alionyesha dhamira hiyo “kuhamia’ Dodoma kama njia ya kuunga mkono.
Historia ya kuhamisha miji mikuu ilitokea miaka ya 1970 nchi nyingi za kiafrika zilibadili miji mikuu ya serikali. Mathalani Malawi ambayo ilibadilisha mji mkuu kutoka Blantyre kwenda jiji la Lilongwe,na Nigeria ilihama kutoka Lagos kwenda Abuja.
Hoja kubwa iliyopelekea Mwalimu Nyerere kuchagua mkoa huo ni kwamba Dodoma ni katikati mwa Tanzania, hivyo itarahisisha kuleta maendeleo katika mikoa yote kwa urahisi hususan utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi. 
Hiyo ndio hoja ya msingi iliyomsukuma Mwalimu Nyerere kutoa maamuzi hayo ambapo alikuwa na uhakika iko siku dhana yake itatimia, Hongera Rais Dkt. John Pombe Mangufuli kwa jitihada zako za kutimiza ndoto za Muasisi wa taifa hili, sote tunaziona juhudi zako na Watanzania wanakuunga mkono, Hapa Kazi Tu”.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.