Habari za Punde

SERIKALI KULILIPA SHIRIKA LA POSTA SH. BIL 3.2

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali imeahidi kuwa italirejeshea Shirika la Posta Tanzania kiasi cha shilingi bilioni 3.2 ambazo ilizitumia kuwalipa wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki ifikapo  kufikia 30 Juni mwaka huu itakuwa imelipa kiasi cha Sh. Bil.3.2 zinazodaiwa na Shirika la Posta Tanzania
Ahadi hiyo imetole Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na MIpango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ludewa, Mhe. Deo Ngalawa (CCM), aliyehoji Serikali ilikuwa na mpango gani wa kuwalipa Wastaafu hao yenyewe moja kwa moja bila ya kutumia fedha za mfuko wa Shirika hilo.
‘’Shirika linasuasua kujiendesha, fedha ambazo zilikuwa zitumike kwenye operation ndizo hizo zimekuwa zikitumika kuwalipa Wastaafu wa Afrika Mashariki ili kulinusuru Shirika hilo serikali haioni umuhimu wa kulipa deni hilo”.alihoji Mhe. Ngalawa.
Mhe, Ngalawa alitaka kujua kwanini Mamlaka ya Mapato  Tanzania (TRA), mwaka 2016 ilifungia akaunti za Shirika la Posta Nchini, kutokana na kuliidai Shirika hilo  kiasi cha  Sh. Mil.600, ikiwa Shirika hilo linaidai Serikali kiasi cha Sh. Bil.5.
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji  alisema kuwa, Serikali ipo kwenye mchakato wa kuhakikisha fedha hizo zinalipwa na Serikali yenyewe na sio Shirika.
Aliongeza kuwa watumishi wote wa Shirika hilo wamekwisha jiunga na mifuko ya Hifadhi ya Jamii, na wanachangia katika mifuko mbalimbali hivyo wakistaafu mifuko hiyo itakuwa ikiwalipa mafao yao na si Serikali tena.
Naibu waziri huyo aliongeza kuwa Serikali itaendelea kulipa madeni hayo kadri fedha zitakapopatikana, watahakikisha ifikapo Juni 30 mwaka huu fedha zote zinazodaiwa  na Shirika hilo zitakuwa zimelipwa.
Katika swali la msingi, Mhe. Ngalawa , alitaka kujua mpango wa Serikali wa kulirejeshea Shirika fedha ambazo lilitumia kuwalipa Wastaafu waliokuwa Shirika la Posta na simu la Afrika Mashariki, kunusuru Shirika hilo.
Akijibu hoja hiyo Dkt. Kijaji alikiri kuwa Shirika limekuwa likitumia fedha zake kuwalipa Wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki na kuwasilisha madai Serikalini ili lipate kurejeshewa fedha zake.
Aliongeza kuwa hadi sasa Shirika limelipa Sh. Bil. 5.9 na Serikali imesharejesha kiasi cha Sh. Bil. 2.7, alisema malipo hayo yamekuwa yakilipwa kwa awamu ambapo kwa mwezi Novemba 2016 kiasi cha Sh. 700,000,000, Desemba 2016 Sh. 1,000,000,000 na Januari 2017 Sh. 1,000,000,000.
Dkt. Kijaji amesema pia kuwa  Serikali itaendelea kurejesha kiasi kilichobaki cha Sh. 3,200,000,000  kadri fedha zitakavyopatikana.
‘Serikali kupitia Msajili wa Hazina inaendelea na jukumu la kuwalipa Pensheni ya kila mwezi Wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki wapatao 292’. Aliongeza Dkt. Kijaji.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.