Habari za Punde

SERIKALI YAFAFANUA JUU YA KUAJIRI ZA MADAKTARI WA TANZANIA WALIOKUWA WAENDE NCHINI KENYA

SERIKALI YAFAFANUA JUU YA KUAJIRI MADAKTARI WALIOKUWA WAENDE NCHINI KENYA, HATUA ILIZOCHUKUA JUU YA CHANGAMOTO ZITOKANAZO NA AGENDA YA MABADILIKO YA UMOJA WA ULAYA NA UKARABATI WA NYUMBA ZA NHC NCHINI.

Serikali imefafanua kuhusu hatua ilizochukua juu ya kuajiri madaktari waliokuwa waende nchini kenya, Changamoto zitokanazo na Agenda ya Mabadiliko ya Umoja wa Ulaya na ukarabati wa nyumba za NHC nchini. Ufafanuzi huo umetolewa leo mjini hapa.

Madaktari waliotakiwa waende Kenya waajiriwa na Serikali 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli ameamua kuwa madaktari 258 na wataalamu wa Afya 11 walioleta maombi na kukidhi vigezo kupitia Wizara ya Afya kwa ajili ya kwenda kufanya kazi nchini Kenya kuajiriwa na Serikali.
Akifafanua suala hilo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu amesema makubaliano ya ratiba ya utekelezaji wa ajira hizo za madaktari hao ilikubalika na pande zote iwe tarehe 6 Aprili 2017 na Madaktari hao wawe tayari kusafiri kwenda nchini Kenya kati ya tarehe 6-10 Aprili 2017, hadi tarehe ya Taarifa hii Mahakama nchini Kenya haijaondoa pingamizi lililofunguliwa kuhusu Ajira za madaktari wa Tanzania nchini Kenya.
Amesema kufuatia uamuzi huu majina ya Madaktari husika na vituo watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika Tovuti ya Wizara pamoja na wataalamu wengine wa afya 11 walioleta maombi yao na kukidhi vigezo.
Aidha Serikali ya Tanzania itakuwa tayari kushughulikia upya ombi la Serikali ya Kenya kupatiwa Madaktari 500, pale ambapo hakutakuwa na vikwazo vya kupeleka madaktari wetu nchini Kenya.
Mnamo tarehe 18 Machi 2017 Ujumbe wa Serikali ya Kenya ukiongozwa na Waziri wa Afya Dkt.Cleopa Mailu uliwasili nchini ambapo ulikutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli kwa madhumuni ya kuomba kuajiri kwa Mkataba Madaktari wa Tanzania mia tano(500) ili kupunguza uhaba wa Madaktari nchini Kenya na kukubali ombi hilo.
Aidha maombi hayo yalipokelewa ambapo jumla ya maombi 496 yaliwasilishwa na baada ya kufanya uchambuzi ilibainika kuwa Madaktari 258 walikidhi vigezo vilivyotakiwa kwenda kufanya kazi nchini Kenya. Lakini wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea kukamilisha utaratibu wa ajira za Madaktari hao Madaktari watano wa Kenya waliwasilisha pingamizi mahakamani kuitaka Serikali ya nchi yao kusitisha kuajiri Madaktari kutoka Tanzania.
Changamoto zitokanazo na agenda ya mabadiliko ya Umoja wa Ulaya.
Serikali imesema kuwa imechukua hatua mahsusi katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na Agenda ya Mabadiliko ya Umoja wa Ulaya.
Akifafanua hoja hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Suzan Kolimba amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali ambazo ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kusimamia matumizi ya fedha za umma ili kuhakikisha tunapunguza utegemezi kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Pia Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuzingatia Sera ya Ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi ya mwaka 2009 na sheria ya Ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi ya mwaka 2010. Imebainishwa kuwa mkakati huu unasaidia kuongeza wigo wa vyanzo za fedha za kugharamia miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi kwa wahisani.
Hata hivyo Serikali inaendelea kuwashawishi wawekezaji kutoka nchi mbalimbali kuja kuwekeza zaidi nchini na zinaenda sambamba na uboreshaji wa mazingira ya kufanyia biashara nchini na kupunguza gharama za kufanya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi kuwekeza nchini.
Katika kuratibu uhamasishaji wa watanzania waishio ughaibuni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeanzisha Idara maalum ya kuratibu masuala ya Diaspora ili kushiriki katika Maendeleo ya Nchi ikiwemo kuwekeza nchini.

Serikali kuendelea na ukarabati wa nyumba za NHC.
Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema kuwa Shirika la Nyumba nchini(NHC) limeweka mkakati wa kuhakikisha nyumba zote zilizo katika hali ya uchakavu zinafanyiwa ukarabati mkubwa na zile ambazo kiwango cha uchakavu ni kikubwa zinavunjwa na kuendeleza upya viwanja hivyo.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Angelina Mabula amesema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeshafanya uhakiki wa nyumba zake zote na kubaini hali halisi ya kila nyumba na kuweka mpango wa kuzifanyia ukarabati nyumba hizo kwa awamu.
Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2016/17 shirika lilitenga takribani shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kuzifanyia ukarabati nyumba zake ambapo hadi mwezi Machi, 2017 jumla ya nyumba 2451 zilikuwa zimekwishafanyiwa ukarabati kupitia bajeti hiyo.
Aidha amesema kuwa shirika hilo linatarajia kumaliza ukarabati wa nyumba zote katika mwaka wa fedha 2017/18 na kusisitiza kuwa matengenezo ya nyumba hizi ni kazi endelevu kwa shirika hivyo bajeti ya matengenezo itaendelea kutengwa kila mwaka ili wapangaji wa nyumba za shirika waendelee kuishi katika nyumba na mazingira bora. 

Imetolewa na:
Idara ya Habari-MAELEZO.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.