Habari za Punde

WAZIRI MWAAKYEMBE AWATAKA TRA KUTUMIA BUSARA KUDAI DENI LA TFF

 Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar
WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, ametoa siku mbili kwa Mamlaka ya Mapato  nchini (TRA) kukaa chini na kumalizana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  kwa kushughulikia na kupata ufumbuzi wa jinsi ya kudai madeni na zaidi kutumia busara katika njia za kudai madeni hayo.
Mwakyembe aliyasema hayo jana usiku katika hafla ya Chakula cha jioni kwa Vijana wa Serengeti Boys kilichoandaliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, iliyofanyika kwenye makazi ya Makamu wa Rais Oysterbay, jijini Dar es Salaam ikiwa ni maalumu kuwaaga na kuwatakia kila la kheri wachezaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys wanaoondoka nchini leo kuelekea Morocco kuweka kambi ya mwezi mmoja kujiandaa na fainali za Afrika nchini Gabon mwezo ujao.

''Namuagiza Katibu Mkuu wa Wizara yangu, akutane na Katibu wa Wizara ya Fedha wakakae na Kamishna Jenerali wa TRA ndani ya siku mbili wazungumze juu ya hili ili angalau kupata muafaka wa tatizo hili, japo wote ni Serikali lakini sidhani kama njia waliyotumia kudai tena kwa kusubiri vijana wameitwa na mkuu wa nchi kama ni sawa,
''Naomba niyaseme haya mbele yako Mheshimiwa Makamu wa Rais, na iwapo itashindikana wakubwa hawa kukutana na kupata muafaka basi, nitakuja kushitaki tena kwako,  
“Ninaogopa nisipoyasema haya mapema (TRA), watakuja kukamata basi wakati linakwenda Uwanja wa Ndege tukachelewa ndege ya kwenda Morocco,”.  Dkt. alisema Mwakyembe
Dk. Mwakyembe alisema anachukua hatua hiyo kwa sababu baada ya kulifuatilia deni hilo la TRA kwa TFF linaonekana ni Serikali. 

Dkt. Mwakyembe alisema hayo baada ya kupata taarifa na kuona katika mitandao ya Kijamii kuwa TRA kupitia kampuni ya udalali na minada ya Yono kukamata basi la timu ya taifa, Taifa Stars lililokuwa limewapakia vijana wa Serengeti Boys, kuelekea nyumbani kwa Makamu wa Rais walikoalikwa Chakula cha jioni na kushushwa katika basi na hatimaye kutafutiwa usafiri mwingine wa kukodi ili kufika katika mwaliko wao.
Mashuhuda wa Ilielezwa kuwa  basi hilo lilichukuliwa nje ya hoteli ya Urbun Rose, Kisutu, jijini Dar es Salaam wakati likiwa linawasubiri wachezaji hao waliokuwa tayari wamepiga sare zao ili liwapeleke nyumbani kwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu.

Hatua hii inakuja kiasi cha wiki tatu baada ya TRA kupitia Yono pia kuzifunga ofisi za TFF kutokana na deni kubwa la muda mrefu la Sh. Bilioni 1.2 linatokana na kodi za mishahara ya waliokuwa makocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo na Mdenmark, Jan Borge Poulsen kuanzia mwaka 2016 hadi 2010.
Tayari TFF chini ya Rais wake, Jamal Malinzi imefanikiwa kulipa deni la zaidi ya Sh. Milioni 400 kodi ya Ongezeko la Thamani (VaT) la ziara ya timu ya taifa ya Brazil nchini mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.