Habari za Punde

FAINALI KOMBE LA FA KUPIGWA UWANJA JAMHURI MJINI DODOMA

BAADA ya sintofahamu iliyotawala vichwani mwa mashabiki wengi wa soka kuhusu ni wapi zitapigwa fainali za Kombe la FA, hatimaye kitendawaili hicho kimeteguliwa na Shirikisho la Soka nchini TFF waliotangaza uwanja utakaopigwa fainali hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari Rais wa Shirikisho hilo, Jamal Malinzi, alisema kuwa uwanja utakaotumika kwa fainali ya michuano ya kombe la FA kati ya timu za Simba na Mbao FC kuwa ni uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
''Mchezo wa Fainali za kuwania Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup HD - ASFC), kati ya Simba SC ya Dar es Salaam na Mbao FC ya Mwanza, utachezwa Mei 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma''. alisema Malinzi
Kwa mujibu wa kanuni, Simba ndio wenyeji wa mchezo huo kwa sababu ndio walitangulia kutinga fainali hizo kwa kuwafunga Azam bao 1-0, kwenye mchezo wa nusu fainali kabla ya Mbao walioichapa Yanga bao 1-0 kwenye mchezo wa pili wa nusu fainali katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Rais Jamal Malinzi alitangaza uwanja huo wakati wa ufunguzi wa kozi ya awali ya makocha na waamuzi iliyoandaliwa na chama cha soka wilaya ya Ubungo, Dar es salam, leo.
Awali Malinzi alisema kuwa, kungefanyika droo ya kupata uwanja kwa ajili ya fainali hiyo ambapo iliibuka mijadala mikubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uhahali wa jambo hilo kutokana na kanuni za michuano hiyo kutoainisha kuhusu taratibu za kupata uwanja kwa ajili ya fainali.
“Natangaza rasmi fainali ya michuano ya kombe la FA kati ya Simba kutoka Dar es Salaam na Mbao kutoka Mwanza itafanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma ili kupata usawa wa pande zote.
Siku ambayo tunafanya droo ya nusu fainali, hili jambo lilisahaulika na ndio maana nikaona ifanyike droo kwa ajili ya kupata uwanja wakuchezea fainali hizo, lakini nilipata taarifa uwanja wa taifa utafungwa mara baada ya kumalizika ligi kuu tarehe 21, kwa ajili ya matengenezo yatakayohusisha kung'oa nyasi zote hivyo tarehe 28 hivyo uwanja hautapatikana na ndio maana nimeona mchezo huo ufanyike Dodoma,”alisema
Hata hivyo Malinzi aliipongeza Simba na Mbao kwa kutinga hatua ya fainali ya kombe hilo na kuwatakia mchezo mwema na yeyote atakayeshinda aweze kushiriki vyema mashindano ya kimataifa na kuipeperusha vyema benderea ya nchi.
“Nawapongeza Simba na Mbao kwa hatua waliyofikia, pia yeyote atakayeshinda aweze kushiriki vyema mashindano ya kimataifa lakini pia waamuzi watakaochaguliwa waweze kuchezesha kandanda safi bila ya uonevu,” alisema

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.