Habari za Punde

SERIKALI KUJENGA DARAJA LA JUU ENEO LA BONDENI JESHINI

Na Daudi Manongi-MAELEZO, DODOMA.
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano imesema itajenga daraja la juu kwa ajili ya kivuko cha waenda kwa miguu(Over head Pedestrian Bridge) eneo la Kawe Bondeni.
Hayo yamesemwa Bungeni leo na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe.Isack Kamwelwe aliyekuwa akijibu swali la Mbunge wa Kawe Mhe.Halima Mdee kwa Niaba ya Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano. 
“Tatizo la kivuko cha waenda kwa miguu eneo la Kawe Bondeni hadi Jeshini Kata ya Mbezi Juu na Kawe Tayari limeshapatiwa ufumbuzi”,Aliongeza Mhe.Kamwelwe.
Amesema kwa sasa Mkandarasi wa kujenga daraja hilo yupo kwenye hatua za maandalizi ya kuanza ujenzi katika eneo hilo muhimu.
Aidha Serikali ina mpango wa kuweka taa za kuongozea magari katika Barabara ya Mwenge-Tegeta ambapo Mkandarasi ameshapatikana wa kuweka taa hizo katika makutano ya Afrikana na anatarajia kuanza kazi wakati wowote.
Mbali na Hayo tatizo la Udogo wa mapokeo na matoleo ya maji ya mvua yanayosababisha kero katika eneo la Makonde hadi Mbuyuni,Serikali inakamilisha taratibu za kusaini mkataba wa ujenzi wa mtaro mkubwa eneo la Mbezi Samaki ambao utatatua kero ya barabara kujaa maji nyakati za mvua.
“Serikali ya Awamu ya Tano ni makini sana na itahakikisha changamoto hizi inazifanyia kazi ili wananchi waweze kutumia barabara zetu vyema”Aliongeza Mhe.Kamwelwe.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.