Habari za Punde

SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI, WAANDISHI WATAKIWA KUTUMIA KALAMU ZAO VIZURI.

Na Nuru Juma & Husna Saidi- MAELEZO
Waandishi wa Habari nchini wametakiwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za uandishi katika kuandika habari zitakazoleta umoja, mshikamano na maendeleo na siyo uchochezi ili kujenga jamii bora.
Hayo yamesemwa leo Jijini Mwanza na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Harrison  Mwakyembe kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.
Dkt. Mwakyembe aliongeza kwa kusema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa siku ya uhuru wa vyombo vya habari ambapo siku hiyo huwa maalum kwa wadau wa tasnia hiyo kukutana na kujadiliana mambo mbalimbali ikiwa ni njia ya kujenga jukwaa la ushirikiano.
“Uhuru wa habari una ukomo wake hivyo ni muhimu kwa vyombo vya habari hapa nchini kuajiri watu wenye taaluma hiyo kwa kuachana na makanjanja ili viheshimike kwa kutoa taarifa zenye kuzingatia maadili ya uandishi”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Alizidi kufafanua kuwa katika kuadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, kalamu ya mwandishi wa habari itetee ukweli na si mambo ya haramu kwa sababu ya siasa au rushwa ambayo huwa kichocheo cha uvunjifu wa amani.
Aidha aliitaka Idara ya Habari (MAELEZO) kuwa na utaratibu wa kukutana na wahariri kila mwezi ili kuweza kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia nzima ya habari nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi alisema uandishi wa habari si biashara ya kawaida bali ni kazi yenye kuhitaji uweledi mkubwa hivyo waandishi wanatakiwa kufuata taratibu na sheria za uandishi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.