Habari za Punde

WAZIRI MWAKYEMBE AKABIDHI BENDERA YA TAIFA KWA TIMU YA AZANIA KWENDA KUSHIRIKI KOMBE LA STANDARD CHARTERED UINGEREZA

 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akimkabidhi bendera Kapteni wa timu ya Azania Khalid (katikati) ambayo inatarajia kusafiri  kwenda nchini Uingereza kushiriki mashindano ya kombe la Standard Chartered, kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko ya Fedha za Kigeni wa Benki ya Standard Charted  Abdulrahman Said.
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) akiongea  katika hafla ya kukabidhi Bendera ya Taifa Timu ya Mpira wa Miguu ya Azania inayoenda kuiwakilisha Tanzania katika Michuano ya kombe la Standard Chartered nchini Uingereza, kulia ni Balozi wa Uingereza nchini Bibi. Sarah Cooke.
 Nahodha wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Azania Khalid Sultan akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhiwa bendera iliyofanyika Jijini Dar es Salaam tayari kwa safari ya kuelekea nchini Uingereza kwa ajili ya Mashindano ya Kombe la Standard Chartered.
 . Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akimkabidhi nyaraka za kusafiri mchezaji wa timu ya Azania tayari kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kombe la Starndard Chartered nchini Uingereza.
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akimkabidhi vifaa vya michezo mchezaji wa timu ya Azania Brian Mhapa tayari kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kombe la Standard Chartered nchini Uingereza. 
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa timu ya Azania pamoja na uongozi wa benki ya Standard Chartered  baada ya halfa ya kukabidhi bendera kwa timu hiyo tayari kwa mashindano ya kombe la Standard Chartered nchini Uingereza. Picha Na Lorietha Laurence
*******************************************************
Na: Genofeva Matemu – WHUSM
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe Dkt. Harrison Mwakyembe ameikabidhi Bendera ya Taifa Timu ya Mpira wa Miguu ya Azania inayoenda kuiwakilisha Tanzania katika Michuano ya kombe la Standard Chartered nchini Uingereza.
Akizungumza jana Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuiaga timu hiyo Mhe. Mwakyembe amewataka vijana wa Timu hiyo kukumbuka kuwa ni muda wa kuonyesha uwezo na vipaji walivyonavyo na kuvitumia kuiletea nchi heshima na kuitangaza katika mataifa mengine duniani.
“Kuwa mabingwa na kuweza kuiwakilisha Afrika Mashariki kuwania kombe la Standard Chartered mmeonyesha uwezo wa hali ya juu, naamini mtatumia uwezo huo  kufanya vizuri zaidi katika michuano hiyo.”Amesema Mhe. Mwakyembe.  
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Benki ya Standard Chartered Tanzania Balozi Ami Mpungwe amesema kuwa Timu ya Azania ina uwezo kwani imefanya vizuri hapa nyumbani katika  michuano ya kitaifa na kanda ya Afrika Mashariki ili kuhakikisha  wanapata ubingwa ambao umewawezesha kusonga mbele na kuitoa  Kenya ambao ndio mabingwa watetezi.
 Naye Balozi wa Uingereza Tanzania Mhe. Sarah Cooke amewataka wachezaji hao  kupambana  kwa ari na uwezo  mkubwa na kanda nyingine za nchi za Afrika pamoja na mabara mengine wakiwa na lengo la kurejea nchini na ushindi ili kuitangaza nchi yetu kupitia kombe la Standard Chartered.
Michuano ya kuwania kombe la Standard Chartered inahusisha nchi zote ambazo Benki ya Standard Chartered ina matawi ambapo kwa Tanzania Timu ya Azania inashiriki na mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Mei 21 mwaka huu katika viwanja vya Anfield nchini Uingereza.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.