Habari za Punde

AJIBU KATI YA MILIONI 60 NA MILIONI 40 UNADHANI NI IPI YENYE FAIDA KWAKO KWA SASA???

Na Abdul Mkeyenge, Dar
RAFIKI yangu Ibrahim Ajib anawavuruga sana Simba siku hizi. Ni kama amewageuza mateka wake. Wiki mbili zilizopita nilikaa nae ndani ya basi tukitokea Dodoma, katika mazungumzo yetu ya kawaida inaonyesha wazi hajutii kuikacha Simba na kuhamia kwingine. Hawa ndio wanasoka wa kileo.
Ajib anataka fedha nyingi asaini mkataba mpya klabuni baada huu wa sasa kumalizika. Kelele zote tunazozisikia kumuhusu yeye, Simba na Singida United ni kutokana na kutaka fedha nyingi. Misingi ya kelele inaanzia hapa.
Simba wanataka kumbakisha mchezaji, lakini mchezaji mwenyewe haonyeshi kuwahitaji Simba kwa wakati huu ndio maana mpaka sasa hajasaini nao mkataba na anawasikilizia Singida United waliomuahidi kumpa fedha nono.
Simba wamekwama kwenye kitanzi hiki cha Ajib na hawana cha kumfanya zaidi wanamtazama kama wanavyowatazama Jonas Mkude na Abdi Banda waliomaliza mikataba na wao wakitaka fedha nyingi wasaini mikataba mipya. 
Simba imefikia hapa na wachezaji wake.
Milioni 60 zinazotajwa ametengewa Ajib na Singida United ni fedha nyingi mno kwa maisha ya kileo ya Kitanzania haswa wakati huu wa bajeti ya nchi iliyotoka. Hii ni fedha nyingi ambayo si Ajib peke yake angeweza kuiwaza mara mbili, hata mimi ningetulia kuiwaza kabla kuifanyia maamuzi, lakini hii ni fedha inayokwenda kumrudisha Ajib hatua kumi nyuma kutoka sasa.
Inawezekana Ajib haipendi Simba, ameichoka, ameikinai na anahitaji changamoto mpya nje ya Simba. Inawezekana kuna kimoja kati ya hapo kinamuondoa Simba, lakini hili lisimfanye atoke Simba na kuhamia Singida United.
Siwabezi Singida United. Nawaheshimu kama moja ya timu itakayoufanya msimu ujao kuwa wa kuvutia, lakini Ajib anatakiwa kufikiri zaidi ya Singida United licha ya kuwa wanampa fedha nyingi zinazompa kiburi cha kufanya asipokee simu za viongozi wa Simba. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Ushauri wangu wa bure ambao ni tija kwa mafanikio yake na soka la Tanzania kiujumla kama anaondoka Simba akajiunge na Yanga au aondoke kabisa nchini. Uwepo wake kwa Yanga inayoshiriki michuano ya kimataifa kama ilivyo Simba inaweza kuwa njia nyepesi kuzikanyaga kwa kishindo nyayo za Samatta.
Samatta aliwatumia Simba kujiuza dhidi ya Mazembe na sasa tunamtaja kama shujaa wa Tanzania kwenye soka. Ajib hawa Singida United wamekupa nini cha ziada kilichokuvutia kutaka kujiunga nao na kuzidengulia Simba, Yanga zenye tiketi ya michuano ya kimataifa mikononi mwao?
Uwepo wa Ajib, Simba au akijiunga Yanga unaweza kwenda kutengeneza fedha nyingi zaidi ya Milioni 60 anazotaka kupewa Singida United. Huku kwa Simba, Yanga anahitaji kuwa na akili ndogo tu. Anasaini mkataba kwa ajili ya kujiuza kupitia michuano hii inayoshiriki. Hii ni akili ya kawaida tu.
Hizi Milioni 40 za sasa zinaweza kwenda kutengeneza Mabilioni ya shilingi kama mwenyewe ataamua. Ajib ana kipaji murua ambacho hakihitaji tume ya Mchanga wa Makinikia kukichunguza. Wachezaji wa aina yake wanatafutwa kila pembe ya dunia tena wananunuliwa kwa fedha nyingi, kwanini aamue kuiweka kando bahati hii na asubiri mechi za Simba, Yanga kama Kombe la Dunia lake akiamua kwenda huko Singida United?
Ni ngumu mchezaji kuonekana kwenye macho ya mawakala akiwa anacheza Singida United. Ajib anatakiwa kulijua hili mapema kabla hajashika peni na kusaini mkataba. Kama hana mipango ya mbali kuhusu soka lake Singida United ni sehemu sahihi ya kwenda, lakini kama anawaza siku moja kuwa Samatta mwingine aipuuze ofa ya Singida United na haraka asaini Simba, Yanga au aondoke nchini.
Mafanikio ya Samatta hayakuja kama uyoga unavyoota sehemu zenye umande. Kuna wakati alikaa na kusema na Serikali yake 'kichwa' kisha kuja na maamuzi ya kikubwa 
yanayomfanya leo tumuone kama mchezaji wa tofauti nchini.
Ajib anahitaji aina ya maamuzi haya ya kikubwa kama ya Samatta na sio maamuzi ya kivulana kama aliyowahi kuyafanya uncle Mrisho Ngassa wakati ule wa majaribio yake West Ham. Licha ya uncle kukosa nafasi ile lakini safari yake kucheza ulaya ilitakiwa kuanzia pale kwa kuzurura sehemu nyingine, lakini haikuwa hivi badala yake aliamua kurudi Tanzania kwa mbwembwe na baada ya siku kadhaa akafunga ndoa. Kupanga ni kuchagua.
Natamani siku moja nimuone Ajib aliko Samatta au akaribie. Nalitamani sana hili litokee, lakini kwa hali ya mambo naona wazi kulisubili hili litokee ni kama nimesimama Ubungo na kusubiri ndege niende kwetu Rufiji.
Nimkumbushe tu Ajib maana kama kujua hata yeye anajua. Kuna wachezaji wengi huwa wanaenda Simba, Yanga wakitaka kusaini bure, lakini wakiwa na malengo ya kufika mbali. Ni uamuzi wako Ajib na Serikali yako kichwani. Ukiamua kubaki Simba sawa, ukiamua kuondoka na kuhamia Singida United ni sawa pia.
Ajib zungumza na moyo wako kabla ya kufanya maamuzi. Idengulie Simba kadri unavyoweza kuwadengulia, lakini kaa ukijua zile Milioni 40 zao zina maana kubwa sana kuliko Milioni 60 za Singida United.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.