Habari za Punde

WATANZANIA WAASWA KUJITOKEZA KUCHANGIA DAMU

NA WAMJW DAR ES SALAAM. 
WATANZANIA waaswa kujitokeza kuchangia damu mara kwa mara ili kuondokana na tatizo la vifo vinavyotokana na upungufu wa damu hasa kwa kina mama wajawazito nchini wanaopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua. 
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipotembelea katika tukio la uchangiaji damu lililofanyika Makao makuu ya benki ya KCB jijini Dar es salaam. 
“Marufuku kwa mtoa huduma yeyote wa afya kuuza damu mgonjwa kwani wananchi wanachangia damu bure kwa manufaa yao ya baadae aidha kwa wao wenyewe au ndugu zao” alisema Waziri Ummy. 
Aidha Waziri Ummy amewaagiza Waganga Wafawidhi wa mikoa kuhakikisha wanaweka mabango yanayoonyesha kuwa damu ni bure kwa wagonjwa wote wanaohitaji huduma hiyo bila ya kubagua mwananchi yeyote. 
Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa mwananchi yeyote mwenye umri wa miaka 18, mwanamke asiye mjamzito wala kunyonyesha na asiyekua mgonjwa kama vile kisukari,saratani na mgonjwa wa moyo anaweza kuchangia damu. 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya KCB nchini Bw. Cosmas Kimario amesema kuwa wameamua kuaandaa uchangiaji wa damu ili kuisadia Serikali katika sekta ya Afya hususani katika kupunguza vifo vinavyotokana na upungufu wa damu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.