Habari za Punde

GCLA YATOA ZAWADI KWA WANAFUNZI NA WALIMU BORA WA KEMIA NA BIOLOJIA

Mgeni Rasmi, Prof. Mohamed Kambi, akimkabidhi zawadi ya cheti mwanafunzi Marynas Frederick kwa kuwa mwanafunzi wa Bora kitaifa kwa somo la Kemia kwa upande wa wasichana waliomaliza kidato cha Nne mwaka 2015 kutokea shule ya wasichana ya St. Francis ya Mkoani Mbeya.
 
 Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Mohamed Kambi akizungumza kwenye hafla ya utoaji tuzo kwa wanafunzi na walimu waliofanya vizuri kwenye matokeo ya Kidato cha nne 2015 na kidato cha Sita 2016 iliyoandaliwa na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kufanyika leo Jijini Dar es Salaam kwenye Ofisi za Mkemia huyo. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

 Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. David Ngassapa  akizungumza wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa Wanafunzi na Walimu waliofanya vizuri katika masomo ya Kemia na Baiolojia. Hafla hiyo imefanyika leo kwenye ofisi za Mkemia Mkuu wa Serikali,Jijini Dar es Salaam.
 Wanafunzi waliopatiwa tuzo kwa kufanya vizuri kwenye masomo ya  Kemia na Baiolojia wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Mgeni Rasmi Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Mohamed Kambi (hayupo pichani) kwenye hafla ya kuwapatia tuzo wanafunzi na walimu waliofanya vizuri kwenye matokeo ya Kidato cha nne 2015 na kidato cha Sita 2016 iliyoandaliwa na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kufanyika leo Jijini Dar es Salaam kwenye Ofisi za Mkemia huyo. 
Mgeni Rasmi wa tuzo, Prof. Mohamed Kambi (aliyekaa katikati) pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala, Prof. David Ngassapa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele, wakiwa pamoja na wajumbe ya Bodi ya Wakala, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bw. Hiiti Sillo (wa pili Kulia) na wanafunzi wote waliopatiwa tuzo kwa kufanya vizuri kwenye masomo ya Kemia na Baiolojia kwa Kidato cha Nne 2015 na Kidato cha Sita 2016.
 *****************************************************
Na Sylivester Omary – RS, GCLA
Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imetoa zawadi kwa wanafunzi wa masomo ya Kemia na Baiolojia waliomaliza kidato cha Nne mwaka 2015 na waliomaliza kidato cha Sita mwaka 2016 pamoja na Walimu Bora wa masomo hayo.
Tuzo hizo zimetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Mohamed Kambi kwa niaba ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala katika hafla fupi iliyofanyika leo kwenye Viwanja vya Ofisi za Mkemia viliyopo jijini humo..
Prof. Kambi amesema kuwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imebuni mbinu bora ya kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi hasa Kemia na Baiolojia kwa lengo la kupata wataalam zaidi wa taaluma hiyo kwa miaka ijayo.
Napenda kushkuru Wakala kwa kubuni mbinu bora, sahihi na endelevu ya kuhamasisha vijana wetu kupenda masomo ya sayansi hasa Kemia na Baiolojia hivyo naamini tuzo hizi zinazotolewa leo zitakuwa chachu kwa wanafunzi kupenda masomo ya sayansi “, alisema Prof. Kambi.
Mganga Mkuu wa Serikali ameongeza kuwa, Wizara inaendelea na juhudi za kuhamasisha vijana wengi kupenda masomo ya sayansi ili waweze kuongeza idadi ya wanaodahiliwa katika michepuo ya masomo hayo kwa ajili ya kuongeza wataalam wengi wa kada hiyo nchini.
Amefafanua kuwa, katika kutekeleza majukumu yake, Wizara inazingatia Sera, Mipango na Mikakati mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na Malengo ya Maendeleo ya Milenia na Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025) ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuboresha huduma na kupunguza idadi ya wagonjwa kwa kila mtoa huduma mmoja hivyo vijana watakapokuwa wataalam wa kesho, wataiwezesha nchi kufikia malengo waliyojipangia.
Prof. Kambi ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha waandaaji wa tuzo hizo kuweka msisitizo katika madhara ya matumizi ya dawa za kulevya ambazo zinaweza kuzima kabisa ndoto ya vijana na nguvu kazi ya Taifa iliyojitosheleza kwa manufaa ya Taifa na Mataifa mengine kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. David Ngassapa amesema, Wakala unatambua umuhimu wa taaluma za Kemia na Baiolojia ndio maana Wakala ilibuni njia ya kuwazawadia wanafunzi wanaosomea masomo hayo ili kuinua taaluma hiyo.
Tupo hapa leo hii kuwahamasisha na kutoa zawadi kwa wanafunzi waliofaulu masomo ya Kemia na Baiolojia pamoja na waalimu wao ili kutoa ushawishi kwa wanafunzi na waalimu wengine kupenda masomo ya sayansi, jambo litakalotupatia  wataalamu ambao watasaidia taifa kwa kutumia vema taaluma za Kemia na Biolojia ili kuweza kulinda afya na mazingira ya nchi yetu.” alisema Prof. Ngassapa.
Nae Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele, ameishkuru Serikali kupitia Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kusaidia kutangaza shughuli za Wakala kupitia vyombo vya habari na kufanya wananchi kutambua majukumu ya Wakala.
Zawadi hizo hutolewa kila mwaka ambapo kwa mwaka huu zimetolewa kwa jumla ya wanafunzi 24 na walimu wanne ambao wamekabidhiwa fedha taslimu, vyeti na vitini vya masuala ya Kemia.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.