Habari za Punde

JITOKEZENI KUCHANGIA MATIBABU YA MOYO KWA WATOTO - DKT. TULIA ACKSON

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akiwa amembeba mtoto Zuwena Said (4) aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kusubiri upasuaji wa Moyo. Kushoto ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watoto Naiz Majani.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akimbembeleza mtoto Venance Christopher (14) aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kusubiri upasuaji wa Moyo. Mhe. Dkt. Tulia alitembelea Taasisi hiyo leo kwa ajili ya kuwajulia hali watoto wanaosubiri kufanyiwa upasuaji.
*********************************************
Na Ripota Wetu, Dar
NAIBU Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson amehimiza watanzania hususan viongozi mbalimbali kujitokeza kuwezesha matibabu ya watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo.
Dk. Tulia ametoa rai hiyo leo alipofanya ziara katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo pia alipata fursa ya kumjulia hali mtoto Doreen Sostenes (3) ambaye matibabu yake yamefadhiliwa na Taasisi ya Tulia Trust ambayo anaisimamia.
“Kwa mujibu wa madaktari kuna zaidi ya watoto 500 ambao wanasubiri huduma ya upasuaji wengi wazazi wao hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu, Kila mtoto mmoja ni Sh milioni 2.
“Mimi na Taasisi yangu, tumechagua kugharamia matibabu ya mtoto Doreen nawasihi wale ambao wanao uwezo wa kumsaidia hata mtoto mmoja wajitokeze, kwa kufanya hivyo tutazidi kusaidia wengi, afya zao zitaimarika, wataenda shule, wataelimika na naamini watakuwa msaada mkubwa kwa Taifa letu baadae,” alisema.
Akieleza kuhusu tatizo linalomsumbua mtoto huyo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto, Naiz Majani alisema amezaliwa na tatizo la tundu kwenye moyo.
“Moyo una vyumba vinne, viwili vipo juu na viwili vipo chini, tundu hilo lipo katikati ya vyumba vya juu na chini, na hivyo kusababisha damu ya safi na chafu kuchanganyika,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo ukuaji wa mtoto huyo si mzuri kama ilivyo kwa watoto wa umri wake.
“Lakini magonjwa mengi ya moyo kwa watoto yanatibika na kupona iwapo wanafikishwa hospitalini kwa wakati na matibabu huwa ni upasuaji, bahati mbaya wengi wanafika wakiwa wamechelewa,” alisema.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.