Habari za Punde

KOCHA MAYANJA AWATULIZA WATANZANIA KUELEKEA MCHEZO DHIDI YA LESOTHO LEO USIKU

KOCHA Mkuu wa timu soka ya Taifa, Taifa Stars, Salum Mayanga amejigamba kuibuka na ushindi dhidi ya Lesotho leo usiku katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 utakaochezwa saa 2 usiku Uwanja wa Azam Complex Chamazi, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wandishi wa habari, Mayanga alisema wamefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mchezo huo kwani miezi miwili iliyopita walicheza michezo miwili ya kirafiki pamoja na kambi ya ndani na nje waliyokaa.
“Tunacheza na timu nzuri ambayo msimu uliopita ilionesha kiwango kizuri katika mashindano haya pia nimeangalia mechi ambazo wamecheza nyuma na kugundua udhaifu wao upo wapi,” alisema Mayanga.
Pia Mayanga alisema watacheza kwa kujituma, ufundi na mbinu ambazo wamezifanyia kazi vizuri hivyo ana uhakika wa kutoka na ushindi.
Naye nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta alisema timu ipo vizuri na wachezaji wamejiandaa vizuri kwa mchezo wa leo.
Kwa upande wa Kocha wa Lesotho Moses Malieho alisema wamejiandaa vizuri kwa sababu wanafahamu Tanzania siyo timu rahisi kwani amefuatilia michezo yao ya nyuma waliocheza na Nigeria na Botswana.
“Tumejiandaa kwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Msumbiji na kushinda 1-0 lakini tumekuja kupambana kwani Tanzania siyo timu ya kubeza,” alisema Malieho.
Pia alisema wanajua Tanzania siyo timu ya kubeza kwani ina wachezaji wanaocheza soka Ulaya na kipindi cha karibuni imekuwa ikifanya vizuri.
Kwa mujibu wa daktari wa viungo wa Taifa Stars, Gilbert Kigadya alisemawachezaji wote wako vizuri kasoro Mohammed Hussein 'Tshabalala' aliyeumia kwenye mechi ya kombe la FA wa Simba dhidi ya Mbao FC uliochezwa katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma hivyo hatacheza.
Mechi hii itachezeshwa na waamuzi kutoka Djibout ambao ni Abdillah Mohammed akisaidiwa na Gamaladen Abdi na Farham Salime na mwamuzi wa mezani ni Twagirumukiza Abdulkarim kutoka Rwanda.
Viingilio vya mchezo ni sh. 5000 viti vya kawaida na sh.10,000 VIP.
Tanzania ipo kundi L pamoja na timu za Lesotho, Uganda na Cape Verde na kila timu moja kwenye kila kundi itafuzu katika fainali hizo ambazo zitafanyika 2019 nchini Cameroon.
Mara ya mwisho Tanzania kushiriki fainali hizo ni 1980 nchini Nigeria wakati zikiitwa fainali za Mataifa Huru ya Afrika lakini kwa miaka ya karibuni imekuwa ikiondolewa katika hatua za makundi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.