Habari za Punde

MALINZI NDO BASI TENA URAIS TFF, APELEKWA MAHABUSU NA WENZAKE, WANYIMWA DHAMANA

 Rais wa TFF Jamal Malinzi akiwa ndani ya gari la Polisi kupelekwa Mahabusu leo mchana baada ya kukosa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu yeye na wenzake, Katibu Mkuu Selestine Mwesigwa, Rais wa Simba Evansi Aveva, Geofrey Nyange 'Kaburu' na Mhasibu wa shirikisho hilo.
Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar
WAKATI usahili wa wagombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF, ukianza leo huku Rais wa Shirikisho hilo aliyeomba ridhaa ya kutetea kiti chake, Jamal Malinzi, Katibu Mkuu wake, Selestine Mwesigwa na Mhasibu wake, pamoja na Rais wa Simba Evans Aveva, na aliomba umakamu wa Rais TFF, Geofrey Nyange, wao imebaki ni miujiza tu inasubiriwa ili kuwanusuru ili kurejea kuendelea na mchakato huo.
Uchaguzi huo wa shirikisho hilo umepangwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu mjini Dodoma, huku wagombea hao wao wakipelekwa Rumande leo baada ya kukataliwa dhamana kutokana na makosa waliyosomewa mahakamani hapo hii leo. 
Malinzi na wenzake wamepelekwa mahabusu hadi Julai 3, mwaka huu kufuatia kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika benki ya Stanbic, jijini Dar es Salaam.
Akisoma mashitaka hayo Hakimu mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, Wilbord Mashauri, alisema kwamba hatawapa dhamana hadi atakapoamua kuhusu suala hilo la kufuatia mabishano ya kisheria ya mawakili wa utetezi dhidi ya mawakili wa upande wa Serikali. 
Katika mashitaka hayo, 25 yamekwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.
Kutokana na kupelekwa Rumande hadi Julai 3 na iwapo Makahama haitabatilisha uamuzi wake wa kuwanyima dhamana, maana yake Malinzi hataweza kushiriki uchaguzi wa TFF, kutetea nafasi yake baada ya miaka yake minne ya awali.
Hiyo ni kwa sababu hatashiriki zoezi la usajili wa wagombea, lililoanza jana na linatarajiwa kumalizika keshokutwa jioni.
Baada ya kazi nzuri katika miaka yake minne ya mwanzo, Malinzi amechukua fomu kutetea nafasi yake dhidi ya Imani Madega, Wallace Karia, Fredrick Masolwa, Fredrick Mwakalebela, John Kijumbe, Shija Richard, Ally Mayay na Emmanuel Kimbe, baada ya mgombea mmoja, Athumani Nyamlani aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa TFF kujitoa.
Nyamlani aliwasilisha barua ya kujitoa Juni 25, mwaka huu ikiwa ni siku moja tu tangu Kamati ya Uchaguzi ipitishe jina lake kuwa miongoni mwa wagombea 10 wanaowania nafasi hiyo ya urais. 
Waliojitokeza kuwania Makamu wa Rais na kurejesha fomu wako Mulamu Ng’hambi, Michael Wambura, Geofrey Nyange, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.
Malinzi amefanya kazi nzuri katika miaka yake minne ya awali, ikishuhudiwa kwa mara ya kwanza timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ikifuzu kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika Mei mwaka huu nchini Gabon.
Katika kipindi chake hicho, imeshuhudiwa michuano ya Kombe la TFF ikirejea, Ligi Kuu za Vijana na Wanawake zikianzishwa na mashindano yote yakiwa na udhamini.
Mfumo wa Ligi za chini umeboreshwa na amedhibiti upangaji wa matokeo na mianya yake – mwaka jana akichukua maamuzi magumu ya kutengua matokeo yenye ‘harufu ya upangwaji’ ya Ligi Daraja za Kwanza na kuziadhibu timu zilizohusika, huku timu iliyofuatia ambayo haikufuzu, Mbao FC ya Mwanza ikichukua nafasi ya kwenda Ligi Kuu.
Na ikashuhudiwa Mbao FC ikionyesha ushindani katika Ligi Kuu hadi kufika fainali ya Kombe la TFF, ambako ilifungwa kwa mbinde na Simba 2-1. 
Japo kuna sehemu kama binadamu, Malinzi alikosea, lakini ‘mizani’ ya utendaji wake TFF inaegemea kwenye mazuri, maana yake soka ya Tanzania bado inamhitaji sana.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.