Habari za Punde

TAIFA STARS YAIVA MISRI, KUREJEA NYUMBANI KESHO JUMATANO

Timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania maarufu kwa jina la Taifa Stars, inatarajiwa kuondoka Cairo, Misri usiku wa kuamkia kesho Jumatano kurejea Dar es Salaam, Tanzania ambako inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, siku hiyo hiyo saa 6.30 mchana.
Timu hiyo iliyosafiri kwa ndege wa Ethiopia, ilikuwa jijini Alexandria - Kaskazini kabisa mwa nchi ya Misri ambako ilipiga kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo dhidi ya Lesotho unaotarajiwa kufanyika Jumamosi Juni 10, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi ya Jumanne Juni 6, mwaka huu, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga amesema kwamba kimsingi amefanikiwa katika kile alichopangilia kukifanya akiwa Misri.
“Kwanza kabisa niweze kumshukuru Mungu. Tulisafiri salama na kufanya mazoezi kwa siku saba hapa Misri. Na leo jioni tunanza safari ya kuelekea Cairo kwa ajili ya safari ya kurudi nyumbani. Naam, kambi ilianza tarehe 23 mwezi uliopita pale Dar es Salaam na tukaja kuendelea huku Misri.
“Naweza kusema kuwa nimefanikiwa au tumefanikiwa. Kambi ni nzuri, mazingira ya kambi ni mazuri na tulifika mahali ambako hakuna mtu anayeweza kufanya movement (mizunguko) zozote za kutoka au kuingia kirahisi kwa sababu tulikuwa kwenye kambi ya Hoteli ya Nyota Tano, lakini ni Jeshi.
“Mazoezi ya kawaida ya kiufundi napo tumefanya vema kwa maana wana vitu vyote tunavyohitaji vilipatikana hasa kufanya mazoezi usiku kwa sababu mchezo wetu utakuwa usiku. Nawaomba tu Watanzania waje kuiunga mkono timu yao,” amesema Mayanga.
Naye, Nahodha Msaidizi wa timu hiyo, Himid Mao Mkami, amesema kwamba kambi ilikuwa nzuri yenye mafanikio ambayo matunda yake yatakuja kuonekana katika michezo mbalimbali ya kimataifa ukiwamo wa Jumamosi dhidi ya Lesotho.
Mchezo huo dhidi ya Lesotho umepangwa kuanza saa 2.00 usiku ambako itakuwa ni mechi ya kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi ‘L’ kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika Cameroon.
Mbali ya Lesotho na Tanzania, mataifa mengine katika Kundi ‘L’ ni Uganda na Cape Verde ambao pia wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, mwaka huu watakuwa katika mchezo wa kwanza pia kuwania nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.