Habari za Punde

WAZIRI MAKAMBA AZUNGUMZIA MAADHIMISHO YA SIKU JANGWA

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba (katikati) akiongea na waandishi wa habari juu ya Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na Ukame. Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa hazina Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Faustin Kamuzora na Bw. Timothy Mande Afisa Misitu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Faustin Kamuzora (kushoto) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa utoaji wa tamko la kuadhimisha siku ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, mkutano huo umefanyika leo katika ukumbi wa hazina Dodoma.
*******************************************
TAMKO LA MHESHIMIWA JANUARY Y. MAKAMBA (MB), WAZIRI WA NCHI - OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA KUPAMBANA NA KUENEA KWA HALI YA JANGWA NA UKAME DUNIANI, TAREHE 17 JUNI, 2017
Ndugu Wananchi,
Mwaka 1994 Baraza la Umoja wa Mataifa liliazimia na kuitangaza tarehe 17 mwezi Juni ya kila mwaka kuwa ya maadhimisho ya siku ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame. Kwa kutambua umuhimu wa kuadhimisha siku hii, tarehe 17 mwezi Juni kila mwaka, duniani kote huadhimishwa Siku ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame. Madhumuni ya kuadhimisha siku hii ni kukuza uelewa miongoni mwa jamii juu ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame na umuhimu wa utekelezaji wake duniani, hususan katika nchi zilizoathirika zaidi na tatizo hili la kuenea kwa hali ya jangwa na ukame hasa katika bara la Afrika. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

Ndugu Wananchi,
Tangu mwaka 1994 nchi zilizoridhia Mkataba wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Kimataifa yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na wadau wengine, huadhimisha siku hii kwa kufanya shughuli kadhaa zinazohusu kupambana na tatizo hili. Mkataba huu ndiyo mkataba pekee wa Umoja wa Mataifa unaolenga kupambana na tatizo la uharibifu wa ardhi katika maeneo kame, na kufanya juhudi za kuhifadhi na kuleta matumizi endelevu ya ardhi. Kwa kutambua umuhimu wa Mkataba huu, Nchi zipatazo 193 ulimwenguni zimeridhia utekelezaji wake hadi sasa. Ni wazi kuwa mkataba huu una umuhimu wa pekee kwa nchi kama Tanzania ambayo uchumi wake unategemea ardhi kwa ajili ya kilimo ambacho kinatoa ajira kwa wananchi wengi.
Ndugu Wananchi,
Kauli mbiu ya mwaka huu katika kuadhimisha siku ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame inasema “Ardhi ni Makazi yetu Tuitunze kwa Manufaa ya baadaye” (‘Our Land, Our Home, Our Future’). Kauli mbiu hii inayoadhimishwa mwaka huu ina malengo ya kuhamasisha jamii kuitunza Ardhi kwa kuwa ndiyo makazi yetu hii ikiwa ni pamoja na kuongeza juhudi zaidi kwa ajili ya manufaa ya baadaye kwetu sisi na vizazi vijavyo. Malengo haya yanadhihirisha umuhimu wa utunzaji wa ardhi na udongo kwa ajili ya matumizi endelevu hasa kuifanya iwe na uwezo wa kuzalisha mazao ya kilimo na mifugo na kutoa huduma zingine muhimu kama vile utalii wa wanyamapori, uwindaji, miti, vyanzo vya maji na uwekezaji wa viwanda ili kuleta ustawi wa jamii kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Hali ya uharibifu wa mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji inaongezeka kwa kasi na hivyo kuongezeka kwa tatizo la ukame, upungufu wa mazao ya kilimo na kupungua kwa chakula mara kwa mara na kuongezeka kwa umasikini miongoni mwa jamii. Ukataji wa miti kiholela na uharibifu wa misitu unaosababishwa na utegemezi mkubwa wa binadamu wa kupata mahitaji kutokana na mazao ya misitu pamoja na huduma zingine muhimu, kunazidisha ukubwa wa tatizo hili. Makazi, Mikakati na program zote muhimu za maendeleo ya nchi hufanyika kwa kutumia ardhi. 
Ndugu Wananchi,
Nchi yetu inakabiliwa kwa kiasi kikubwa na hali ya kuenea kwa jangwa na ukame. Takwimu zinaonyesha kuwa takriban asilimia sitini na moja (61) ya eneo la nchi liko katika hatari ya kugeuka jangwa. Miongoni mwa mikoa ambayo imeathirika zaidi ni pamoja na Singida, Dodoma, Shinyanga, Manyara, Simiyu, Geita  na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Arusha. Tayari madhara mbalimbali ya kuenea kwa hali ya jangwa na ukame yameanza kuonekana ikiwa ni pamoja na kukauka kwa vyanzo vya maji katika maeneo mbalimbali, vifo vya mifugo na wanyama pori, upungufu wa mvua kutokana na ukataji wa miti kiholela, migogoro baina ya wafugaji na wakulima kutokana na kupungua kwa maeneo ya kilimo na malisho ya mifugo.
Ndugu Wananchi,
Kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kuna madhara makubwa sana katika uchumi wa taifa letu. Kama inavyoeleweka asilimia themanini (80) ya Watanzania inategemea kilimo ambacho kwa kiwango kikubwa  kinategemea mvua. Kutokana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame ni dhahiri kuwa uzalishaji wa mazao unapungua kwa kiasi kikubwa. Hali hii inachangia kuathiri kushuka kwa uchumi   hasa unaotegemea uuzaji wa mazao ya chakula na biashara. Hali hii itapunguza pia upatikanaji wa kipato katika ngazi ya kaya na ngazi ya taifa kiujumla. Kuenea kwa hali ya jangwa na ukame pia kunasababisha upotevu wa rasilimali zingine kama misitu, vifo vya wanyama pori ambao ni chanzo kikubwa cha fedha za kigeni kupitia utalii. Aidha, kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kunasababisha tabaka la juu la ardhi kuwa wazi na hivyo kutoa nafasi kwa mmomonyoko wa udongo kwa njia ya maji na upepo. Hali hii inasababisha kupungua kwa rutuba katika udongo na hivyo kupunguza uzalishaji wa mazao kwa kiasi kikubwa. 
Ndugu Wananchi
Ili kupambana na hali ya kuenea kwa jangwa na ukame serikali imechukua hatua mbalimbali. Hatua hizo ni pamoja kuandaa taarifa ya hali ya kuenea kwa jangwa na ukame (Status of Land Degradation) ya mwaka 2014; Mpango kazi wa Kitaifa wa Kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame (National Action Program to Combat Desertification) ya mwaka 2014-2018. Taarifa na Mpango kazi huu vimetoa maelekezo mbalimbali kwa mamlaka husika, maelekezo ambayo utekelezaji wake ni wa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Maelekezo haya ni pamoja na programu za upandaji miti, kuandaa mpango wa matumizi bora wa ardhi, kulima kilimo kinachofuata njia za kisasa, ufugaji bora na wa kisasa, kuanzisha maeneo ya hifadhi na kuyalinda yale yaliyopo, kusisitiza matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kuendeleza njia bora kuhifadhi maji na uvunaji wa maji hasa kipindi cha mvua na kuelekeza wananchi kuwa na shughuli zingine za uzalishaji mali (Other income generating activities) ili kupunguza utegemezi katika maliasili. Kwa mfano,  programu ya kitaifa ya upandaji miti ya mwaka 2016 hadi 2021 inalenga kupanda miti zaidi ya milioni 280  kila mwaka na inalenga hasa maeneo yaliyo katika hatari za kukabiliwa na hali ya jangwa na ukame.
Ndugu Wananchi,
Ili kukabiliana na tatizo hili na kwa ajili ya kutunza na kuhifadhi maliasili, Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Kupanda na Kutunza miti wa mwaka 2016 – 2021. Mkakati huu unalenga kupunguza kasi ya uharibifu wa ardhi kwa njia ya kupanda na kutunza miti na kuhakikisha kwamba kila mwananchi anahusika katika utaratibu huu. Aidha, pamoja na mambo mengine, Mkakati wa kupambana na ukame na Jangwa na mikakati mingine ya Mazingira inaendelea kutekelezwa. Pia serikali inaandaa mkakati wa kupunguza matumizi ya nishati ya Mkaa itokanayo na miti ya misitu ya asili. Kuongeza juhudi za matumizi ya Usimamizi Endelevu wa Ardhi. Kufanya Tathmini za Athari kwa Mazingira na Tathmini za Mazingira Kimkakati. Malengo yote haya ni kutaka kufikiwa wadau wote na endapo wadau wote katika sekta ya mbalimbali watahusika katika utunzaji wa mazingira na matumizi endelevu ya Ardhi malengo ya baadaye yatafikiwa.
Ndugu Wananchi;
Matumizi endelevu ya Ardhi, Kupanda na kutunza Miti ni mojawapo ya mikakati inayoweka ulinganifu katika shughuli za kilimo, ufugaji, misitu, uhifadhi wa vyanzo vya maji na kuhakikisha kuwa mifumo ya ikolojia inayotegemeana haiingiliwi. Juhudi hizi zitasaidia katika utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (UNCCD) kwa kuhakikisha kwamba Mpango wa Taifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (NAP) 2014 unakuwa nyenzo muhimu ya kuongeza uzalishaji katika kilimo; kuondokana na tatizo la uharibifu wa ardhi; kuongoa maeneo yaliyoharibika na kurejesha misitu katika maeneo ya nyanda kame; na hivyo kupunguza umasikini.
Ndugu Wananchi,
Ninaomba kutoa rai kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kutekeleza kauli mbiu ya mwaka huu 2017 ya siku ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame ili kuhakikisha ardhi yetu inatunzwa, ardhi iliyoharibika imeongolewa, kwa ajili ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. Hii inawezekana `ikiwa kila mmoja wetu atashiriki kikamilifu katika eneo Lake.

Asanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.