Habari za Punde

MWAKYEMBE AIPA BARAKA TIMU YA RIADHA TAIFA


WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe ameitaka timu ya Taifa ya riadha kuhakikisha inapeperusha vyema bendera ya  Tanzania.
Timu hiyo itashiriki mashindano ya dunia ya riadha yatakayofanyika England  kuanzia Agosti 4 hadi 13 mwaka huu na kushirikisha timu za mataifa 190 duniani
Tanzania itashiriki michuano hiyo na kuwakilishwa na wanariadha wanariadha wanane ambao ni Alphonce Simbu, Ezekiel Ngimba, Stephano Gwandu, Sara Ramadhani,   Magdalena Shauri ambapo watakimbia mbio za nyika huku Gabriel Geay, Emanuel Giniki na Failuna Abdi wakikimbia mbio fupi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, katika halfa ya kuwakabidhi bendera wanariadha hao, Mwakyembe, alisema ni matumaini yake kuwa wanariadha hao wataonyesha viwango vya juu na kuiletea Tanzania medali.
Mwakyembe alisema wizara yake itakuwa bega kwa bega na wanariadha hao kuhakikisha wanashiriki michuano hiyo bila kupata changamoto ya aina yeyote ule. 
Alisema vijana hao wanatakiwa kuonyesha juhudi kwa ajili ya kuiletea heshima nchi yao na ni fursa pia kwao kujitangaza kimataifa.
Aliongeza kwa kusema kuwa uwezo waliouonyesha katika   mashindano mbalimbali ikiwemo ya Olimpiki iliyofanyika  mwaka jana nchini Brazil wanapaswa kuuonyesha pia kwenye michuano hiyo. 
Naye mwanariadha Alphonce Simbu alisema  wamejiandaa vizuri na watahakisha wanapepeeusha vyema bendera ya nchi yao.
"Sisi ni mabalozi wa nchi yetu hivyo hatuna budi kuitangaza kwa kufanya vyema na kunyakua medali," alisema Simbu. 
Simbu aliwataka watanzania kuwaunga mkono na kuwaombea ili waweze kufanikisha ndoto zao.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.