Habari za Punde

MWANAMUZIKI WA MSONDO NGOMA SHABAN DEDE AZIKWA JIJINI DAR ES SALAAM

MWANAMUZIKI gwiji wa uimbaji na utunzi wa nyimbo za dansi nchini, Shaban Dede amezikwa leo katika makaburi ya Kisutu, jijin Dar es Salaam.
Dede alifariki dunia jana, asubuhi, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,  ambako alikuwa amelazwa kwa wiki mbili akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.
Kabla ya kifikwa na umauti, Dede alishazushiwa kifo wiki iliyopita, kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii lakini uongozi wa msondo ulikanusha habari hizo.
Dede alianza kuimba akiwa bendi ya Msongo Ngoma, enzi hizo ikiitwa Juwata Jazz, DDC Mlimani Park, Bima Lee na baadaye kurejea Msondo Ngoma miaka minne iliyopita na alikuwa mmoja wa watunzi mahiri wa nyimbo, hasa alipokuwa bendi ya Mlimani Park, ambapo inasemekana alitunga nyimbo zaidi ya 100, akiwa anashika nafasi ya pili nyuma ya Hassan Rehani Bitchuka.
Kifo cha Dede sio pigo tu kwa familia yake, bali pia kwa wanamuziki wenzake na wengi wakimuelezea bado alikuwa akihitajika kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kutunga na kuimba nyimbo zenye mvuto.
“Ninamfahamu Dede kwa kipindi kirefu kwani alikuwa mtunzi mzuri na mtu mwenye mchango mkubwa katika tasnia ya muziki. Nimesikitishwa sana na kifo chake na pengo lake halitazibika kwa urahisi,” alisema Bichuka, alipozungumza.
Kiongozi wa sasa wa Mlimani Park, Abdalah Hemba, amekiri kuwa Dede ndiye aliyeibua kipaji chake, ambacho kwa sasa kimemfanya awe mwimbaji mahiri na kiongozi wa bendi hiyo kongwe nchini.
Hemba alisema Dede ndiye aliyemsaidia kuingia katika bendi hiyo na kujulikana kupitia sanaa ya muziki na alikuwa mtambuzi mzuri wa vipaji vya wanamuziki baada ya kuwa nao kwa muda mfupi.
Miongoni mwa nyimbo za Dede, ambazo zinapendwa na wadau wa muziki wa dansi ni Fumanizi, Kelele za paka hazimzuii mwenye nyumba kulala, Mshenga, Baba mkwe, Amina, Talaka rejea na Kizabinazabina.
Nyimbo hizo na nyinginezo kadhaa, alizitunga wakati akiwa katika bendi ya DDC Mlimani Park kwa muda wa miaka 27, kabla hajarudi katika bendi yake ya zamani ya Msondo Ngoma, mwaka 2014.
Mbali na wimbo wake wa ‘Suluhu’, ambao ulikuwa wa kwanza kuutunga baada ya kurejea Msondo Ngoma, mwanamuziki huyo pia aliitungia bendi hiyo nyimbo kedekede, ikiwemo Fatuma, Umbea umenichosha, Julekha, Jane, Kuruthumu na Amba ambazo zilimjengea umaarufu na kujikuta akipachikwa jina la ‘Kamchape’ 
Dede alilazimika kurejea Msondo Ngoma kutokana na bendi hiyo kuyumba baada ya kuondokewa na waimbaji wake waliokuwa tegemeo mfululizo, akianza Suleiman Mbwembwe, Othmani Momba, Ally Muhoja Kishiwa ‘TX Moshi’ na Joseph Maina.
Vifo vya waimbaji hao vilisababisha bendi hiyo kongwe kubakiwa na mwimbaji mmoja pekee marehemu Maalimu Gurumo, hivyo uongozi uliona kuna kila sababu ya kumrejesha Dede ili kuongeza nguvu akisaidiana na Eddo Sanga, Juma Katundu na Hassan Moshi.
Uwezo wake wa kutunga na kuimba haukuishia kwa bendi hizo mahasimu kwani alipotua Bima Lee, mwaka 1983, aliwika kwa nyimbo kama Kipepeo, Bilionea wa mapenzi, Shangwe ya harusi, Zenaba, Kununanuna na Dunia duara.
Dede pia aliwahi kung'ara katika bendi ya Orchestra Safari Sound, ambako alivuma kwa nyimbo kama Nyumba ya mgumba haina matanga, Habari imeota mbawa, Titi na Mariam, kabla ya kurejea DDC Mlimani Park.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.