Habari za Punde

WAGOMBEA WAANZA KUJINADI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU WA CHAMA CHA SOKA CHA WANAWAKE JULAI 08

Mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha soka la Wanawake Amina Kaluma akinadi sera zake mbele ya wanahabari.
*********************************************
Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar
KUELEKEA uchaguzi Mkuu wa Chama cha Soka la Wanawake unaotarajiwa kufanyika Jumamosi ya Julai 08 wagombea wa nafasi mbalimbali wameanza kujinadi sera zao wakiahidi kuendeleza vyema soka la wanawake linaloanza kushika kasi kwa sasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wagombea hao wanaotetea nafasi zao wamesema kuwa wanatarajiwa kuendeleza pale walipoishia katika awamu waliyotoka kwani wanaamini kuwa wakirejea katika nafasi zao maendeleo ya soka la wanawake yatazidi kukua.
Mwenyekiti anayetetea nafasi yake, Amina Kaluma amesema kuwa atahakikisha anazidisha mahusiano mazuri na mashirikisho mengine ya soka kutoka nchi tofauti ikiwemo kujitangaza zaidi kwenye soka la wanawake.
Amina amesema kuwa, atatumia nafasi yake kama Mwenyekiti kuwashawishi wakina mama kuwaruhusu watoto wao kucheza mpira wa miguu ikiwemo kuwahamasisha wao kama wanawake kusaidia katika kuinua soka la wanawake kwani asilimia kubwa nao ni mashabiki wa mpira.
"Nitatumia nafasi yangu kuwahamasisha wakina mama kujiwekeza zaidi katika soka la wanawake kwani asilimia kubwa wao ni mashabiki na pia waweze kuwaruhusu watoto wao wa kike kucheza mpira wa miguu kwani
hauna uhuni kama wengi wanavyosema,"amesema Amina.
Kwa upande wa Mgombe wa nafasi ya Katibu Mkuu anayetetea nafasi yake Somoe Ng'itu amesema kuwa katika kipindi chao cha miaka minne iliyopita wameweza kuhakikisha ligi ya wanawake inachezwa na ikiwa katika ubora wa hali ya juu pamoja na kupata udhamini.
Mbali ba hilo wameweza kushiriki katika Kombe la Afrika Mashariki na Kati na kufanikiwa kutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza, TWFA imeweza kuwa na timu za vijana za Taifa kwa upande wa wanawake kwa umri wa miaka 17 na 20 huku kwa mara ya kwanza ikijumuisha wachezaji kutoka nchi nzima.
Uchaguzi wa wanawake utafanyika Jumamosi huku kampeni za Uchaguzi zikiwa zimeanza Julai 4 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.